Tuzo za TFF zawapa kiburi Fountain Gate

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:29 PM Oct 22 2024
Kocha Bora wa Septemba, Mohamed Muya
Picha:Mtandao
Kocha Bora wa Septemba, Mohamed Muya

BAADA ya kutangazwa kuwa Kocha Bora wa Septemba, Mohamed Muya wa Fountain Gate, ameibuka na kusema ataendeleza ubora wake ili kuifanya timu anayoifundisha kuwa bora zaidi na tishio kwa ajili ya kupata tuzo nyingi zaidi, huku timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya KMC jana kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa, Babati mkoani Manyara.

Akizungumza kutoka mkoani humo, Muya ambaye alitangazwa hivi majuzi kuwa kocha bora wa mwezi huo, akiwashinda Rachid Taoussi wa Azam FC na Denis Kitambi wa Singida Black Stars, amesema anajisikia faraja huku akisema si tuzo yake pekee bali ni ya klabu nzima, akimpongeza pia mchezaji wake, Selemani Mwalimu kuwa mchezaji bora wa mwezi huo.

"Ni jambo kubwa sana kwangu mimi na klabu yetu, tuzo nimepata mimi, lakini kazi imefanywa na watu wengi, ndiyo maana utaona hata kile nilichokuwa naelekeza wachezaji kimesababisha straika wangu, Selemani Mwalimu naye kupata tuzo, nampongeza sana, nadhani hii imetupa chachu ya kuendelea kujituma zaidi na zaidi ili tuweze kupata mafanikio, tutapambana ili kuendelea kuzoa tuzo nyingi zaidi zitakazoifanya pia timu yetu izidi kuwa tishio kwenye Ligi Kuu," alisema kocha huyo.

Naye Ofisa Habari wa klabu hiyo, Issa Mbuzi, amesema tuzo tatu walizozipata zinaonesha kabisa kuwa Fountain Gate ni moja kati ya timu tishio nchini, akizionya timu zingine za Ligi Kuu kuwa msimu huu wana lao jambo.

"Hapo ndipo timu zijue kuwa tuna kikosi cha aina gani, tuna mchezaji bora, kocha bora wa mwezi na mchezaji ambaye aliingia fainali na itacheza kwenye uwanja ambao meneja wake naye ametwaa tuzo," alitamba Ofisa Habari huyo.

Mwalimu alitangazwa kuwa mchezaji bora wa mwezi baada ya kuwashinda Feisal Salum wa Azam FC na mchezaji Edgar William pia wa Fountain Gate ambao waliingia nao fainali katika mchakato huo, huku Kamati ya Tuzo ya TFF ikimtangaza Meneja wa uwanja huo, Godwin Israel kuwa meneja bora wa mwezi huo.

Katika mchezo wa jana, straika huyo aliongeza bao lingine, akifikisha mabao sita akizidi kuwa juu ya kilele cha ufungaji bora, huku Edgar akifikisha bao la nne, lingine likifungwa na Dickson Ambundo ambaye sasa ana mawili, huku la kufutia machozi kwa KMC likifungwa na Andrew Vicent.