TFF yazishukia Simba, Yanga

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:19 PM Oct 22 2024
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Wallace Karia
Picha: Mtandao
RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Wallace Karia

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Wallace Karia, amezitaka timu za Ligi Kuu zenye wachezaji walio chini ya miaka 20 na hawapati nafasi za kucheza dakika nyingi, watolewe kwa mkopo kwenye timu zingine zenye mahitaji.

Rais huyo alisema hayo baada ya kumalizika kwa michuano ya Afrika Mashariki na Kati, Ukanda wa CECAFA, ikishuhudiwa Timu ya Taifa ya Tanzania, Ngorongoro Heroes, ikitwaa ubingwa kwa kuifunga Kenya mabao 2-1, katika mchezo wa fainali uliochezwa juzi, Uwanja wa KMC, Mwenge, Dar es Salaam.

Mabao ya washindi yalifungwa na Valentino Mashaka ambaye ni straika wa Simba, na Shekhan Khamisi anayeitumikia Yanga katika nafasi ya kiungo, wote wakiwa hawapati nafasi mara kwa mara katika vikosi vya kwanza vya timu hizo.

Karia alisema wachezaji hao vijana wanapaswa kupata dakika nyingi za kucheza ili wawe bora, wainue viwango vyao na kuwa na utayari kimwili.

"Tunaendelea kuzitunza timu zote za taifa chini ya miaka 17 na 20, na wale wachezaji ambao wapo kwenye timu mbalimbali za Ligi Kuu ambao hawapati nafasi kwenye vikosi vyao, klabu ziwapeleke kwa mkopo kwani zipo ambazo zinahitaji wachezaji, Ligi Kuu na hata Championship," alisema Karia.

Akizungumzia mashindano hayo alisema yalikuwa mazuri na magumu, huku akisifu maandalizi yaliyofanyika.

"Ilikuwa ni michezo mizuri, lakini migumu, Watanzania wamepata burudani pia malengo ya CECAFA yamefikiwa kwa kuandaa na kumaliza salama washindi wakipatikana, sisi kama Watanzania tujipongeze kwa timu yetu kupata nafasi ya kucheza fainali za AFCON kwa vijana 2024/25 na pia kuwa mabingwa, tumerudia historia miaka minne iliyopita nchini Uganda, tulipowafunga Kenya bao 1-0 tukawa mabingwa, nakumbuka wakati huo nahodha alikuwa Dickson Job, Novatus Dismas, Abdul Selemani Sopu na wengineo," alisema rais huyo wa TFF.

Mfungaji wa bao la kwanza, Mashaka alisema alicheza mchezo huo akiwa majeruhi, lakini alikubali kuingia dimbani kwa sababu ya uzalendo.

"Nilicheza nikiwa na majeraha, ilikuwa nisicheze, lakini nikaona hii ni mechi yangu kwa majeraha haya niliyokuwa nayo bado naweza kuingia uwanjani kulipambania taifa, ndiyo maana uliona nilicheza nikapambana nikafunga bao, pale nilipozidiwa nilitolewa na akaingia mtu mwingine," alisema.

Naye Shekhan, alisema amefurahi kufunga bao la pili na la ushindi, akisema awali walianza vibaya michuano hiyo kwa sababu hawakuwa wanaelewana kutokana na kila mchezaji kutoka kwenye timu tofauti.

Tanzania na Kenya, zote zimefuzu kucheza fainali za AFCON chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani kwenye nchi ambayo itatangazwa baadaye.