Stars: Tunajiandaa kulipa kisasi dhidi ya DR Congo

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 12:44 PM Oct 12 2024
Taifa Stars.
Picha:Mtandao
Taifa Stars.

WAKATI kikosi cha Timu ya Taifa (Taifa Stars), kimerejea nchini salama, Kaimu Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hemed Suleiman 'Morocco' amesema wanajiandaa kulipa kisasi katika mechi ya marudiano dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DR Congo).

Stars ilikubali kufungwa bao 1-0 na DR Congo katika mechi ya Kundi H ya kusaka tiketi ya kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2025) iliyochezwa jijini Kinshasa juzi.

Morocco alisema licha ya kupoteza mchezo huo, bado wana nafasi ya kurekebisha makosa yaliyoonekana katika mechi hiyo na kuvuna ushindi watakaporudiana Jumanne kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

"Mechi ilikuwa hamsini kwa hamsini, yoyote angeweza kushinda, kuna kosa tulifanya tumeruhusu goli, tutarekebisha hali hii, mimi kama mwalimu nimeona kuna matatizo mengi ukiachilia mbali hilo la kuruhusu bao,  hayo yameshapita, inabidi tuangalie mbele kwa sababu tunatakiwa kupata ushindi katika mchezo utakaofuata na kulipa kisasi," alisema Morocco.

Kocha huyo alisema bao hilo limetokana na wachezaji wake kupoteza umakini, lakini hana muda wa kukumbuka kilichotokea na siku chache zilizopo atarekebisha mapungufu kabla ya mchezo wa marudiano.

"Tulipoteza umakini tukaruhusu goli, tunarudi kwenye uwanja wa mazoezi kutatua matatizo ambayo yameonekana, kwa kifupi tu narudia, tusahau yaliyopita, hatuna muda, tuna siku chache tu, naamini tutafanya vizuri," Morocco aliongeza.

Alisema sehemu anayoiangalia zaidi kuelekea mchezo unaofuata ni eneo la ushambuliaji na kutengeneza nafasi ili kupata mabao katika mchezo huo na hakuna kingine kinachohitajika zaidi ya ushindi.

"Mimi kama kocha naamini tuna nafasi ya kufuzu AFCON, Watanzania waendelee kutusapoti, tutafanya kila linalowezekana ili tuwafurahishe nyumbani," aliongeza nyota huyo wa zamani wa Stars.

Dakika ya 53, straika wa Stars, Clement Mzize, alijifunga akiwa katika jitihada za kuokoa mpira wa kona.
Matokeo hayo yanaifanya DR Congo kufikisha pointi tisa, ikiwa kileleni katika Kundi H ikifuatiwa na Stars yenye pointi nne huku mchezo wa raundi ya tatu kati ya Guinea dhidi ya Ethiopia unatarajiwa kupigwa leo.