Maxi: Hakuna dabi rahisi duniani kote

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:18 PM Oct 12 2024
Maxi Nzengeli.
Picha:Mtandao
Maxi Nzengeli.

KUELEKEA katika mechi ya watani wa jadi itakayochezwa Oktoba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, kiungo mshambuliaji wa Yanga, Maxi Nzengeli, amesema hakuna dabi rahisi duniani.

Akizungumza jijini jana, Maxi, ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, (DR Congo), amesema mechi yoyote ikishaitwa dabi, ambayo inazikutanisha timu zenye upinzani wa asili huwa ni ngumu bila kujali yupi yuko katika kiwango kizuri kwa wakati huo.

Nyota huyo amesema mechi hiyo haitakuwa rahisi kama baadhi ya watu wanavyodhani, ila kama kupata ushindi kwa upande wao itatokana na uwezo, ufundi, mbinu za makocha wao, pamoja na kujituma.

"Anayesema mchezo huu utakuwa rahisi sijui anafikiria nini, kwangu ni mechi ngumu sana, kwa sababu dabi yoyote duniani huwa ngumu na haitabiriki, ndiyo maana unaona tupo mazoezini, tunafanya mazoezi kwa juhudi na bidii kwa sababu ya kwenda kucheza mchezo huo, kama hata mechi za kawaida tu watu tunafanya mazoezi, iweje leo mtu aseme eti dabi si ngumu, au hata atokee mchezaji aseme eti itakuwa ni kawaida tu, hapana," alisema Maxi.

Mchezaji huyo ambaye ana msimu wa pili katika kikosi hicho alisema kutokana na kujua siku zote dabi huwa ngumu, ndiyo maana tunahakikisha tunapambana ili kufunga mabao.

Aliongeza wanaendelea kujiandaa vizuri na mchezo huo ili kuhakikisha wanashinda mchezo huo.

"Mchezo utakuwa mgumu lakini kwetu ni muhimu kushinda, mimi nimejiandaa vizuri zaidi ya kawaida, nakumbuka mechi zangu mbili za dabi nimefunga," alisema nyota huyo.

Alikiri msimu huu Ligi Kuu imekuwa ngumu zaidi kuliko msimu uliopita kutokana na timu nyingi kusajili wachezaji wazuri na kufanya maandalizi bora.

Maxi aliweka wazi anavutiwa na viungo Awesu Awesu wa Simba, Mudathir Yahaya wa Yanga na Feisal Salum wa Azam FC.

Wakati huo huo, wachezaji wa timu hiyo wamekuwa wakifanya zaidi mazoezi ya utimamu wa mwili kuelekea mechi hiyo ya dabi.

Inaelezwa Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi, amekuwa akisisitiza mazoezi ya 'gym' ili wachezaji wawe na fiziki zaidi kwa sababu anaamini mchezo huo utakuwa na matumizi 'makubwa' ya nguvu kwa nyakati fulani.

Mkongomani huyo tayari amepachika mabao katika dabi mbili ambazo amecheza, akianza Agosti 9, mwaka huu alifunga bao pekee kwenye mchezo huo, huku msimu uliopita, Novemba 5, mwaka jana, akifunga mabao mawili, akiiwezesha timu yake kuibamiza bila huruma, Simba mabao 5-1.

Mabao mengine katika mchezo huo wa msimu uliopita yalifungwa na Kennedy Musonda, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz Ki.