Fadlu awatisha Yanga SC

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 01:09 PM Oct 12 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.

ILI kuhakikisha inapata ushindi katika mechi ya dabi, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema timu yake haitacheza kama ilivyokuwa kwenye mechi ya Ngao ya Jamii kwa sababu kikosi chake kwa sasa kimeimarika zaidi.

Simba ilifungwa bao 1-0 na Yanga katika mechi ya hatua ya nusu fainali ya Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 9, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Wekundu wa Msimbazi watakuwa wenyeji katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Oktoba 19, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Akizungumza jijini jana, Fadlu alisema katika mchezo uliopita timu yake ilipoteza kwa sababu ilikuwa na wachezaji wengi wapya, dabi yao ya kwanza na ndiyo  walikuwa wamekutana huku wakiwa hawajazoeana.

Fadlu alisema mechi hiyo ya dabi iliyopita imewasaidia baadhi ya wachezaji wake 'vijana' kujua mazingira na matakwa ya mchezo huo, hivyo anaamini mchezo unaokuja wapinzani wao watarajie kukutana na 'kitu' tofauti.

"Nafikiri mchezo wetu wa kwanza Ngao ya Jamii ulitusaidia sana, baadhi ya wachezaji wetu walikuwa ni mara ya kwanza kucheza dabi ya Tanzania, nadhani kwa sasa wameanza kuelewa nini maana ya michezo hiyo.

Sidhani kama tunaweza kuingia tena kama vile, wachezaji vijana tayari watakuwa na uzoefu na wataongeza umakini wakishirikiana na nyota wazoefu waliowakuta, wapinzani wetu watarajie kukutana na aina nyingine kabisa ya mchezo pamoja na umakini wa wachezaji wangu tofauti na mechi iliyopita," alisema Fadlu.

Kocha huyo alisema katika mchezo huo hawaendi kulipiza kisasi cha kufungwa mchezo wa kwanza, badala yake wanakwenda kuendelea kupata uzoefu pamoja na kushinda mchezo huo ili kuvuna pointi tatu.

"Hatutaingia kwa kulipiza kisasi, ila kuendelea kupata uzoefu na kushinda kwa ajili ya kupata pointi tatu za Ligi Kuu Tanzania Bara, najua haitakuwa rahisi, lakini tumejiandaa na ugumu ambao tutakutana nao," Fadlu alisema.

Kuhusu kukosekana kwa wachezaji waliopo katika timu mbalimbali za mataifa yao, alisema ni tatizo kwa sababu watajiunga kambini siku chache kabla ya mchezo, lakini si tatizo kwao pekee, hata wapinzani wao, Yanga inawahusu.

"Kutokuwa na baadhi ya wachezaji waliokwenda kwenye vikosi vya timu ya taifa kwenye maandalizi ni tatizo,  lakini hata wapinzani wetu pia wanapitia changamoto hiyo, lakini nitajaribu kufanya kila kinachowezekana ili wawe katika kiwango bora kwa ajili ya mchezo huo," alisema kocha huyo.

Aliongeza kwa sasa anaendelea kuwafua wachezaji waliobakia, akifanya mazoezi mara mbili kwa siku, asubuhi wakifanya mazoezi ya utimamu wa mwili na jioni wanakwenda uwanjani kwa ajili ya mazoezi ya ufundi.

Katika msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Simba yenye pointi 13 iko katika nafasi ya pili nyuma ya vinara Singida Black Stars yenye pointi 16, lakini imecheza mchezo mmoja zaidi.

Mabingwa watetezi, Yanga yenye pointi 12, imecheza mchezo mmoja pungufu ukilinganisha na watani zao na iko katika nafasi ya nne kwenye mzunguko wa ligi hiyo yenye kushirikisha timu 16 kutoka mikoa mbalimbali.

Tayari homa ya mchezo huo imeshaanza, huku wanachama na mashabiki wa timu hizo hasa za mikoani wakianza kuhamasishana kutoka mikoani kusafiri hadi jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kushuhudia mchezo huo ambao Simba itakuwa mwenyeji.