KMKM kileleni Ligi Kuu Zanzibar

By Hawa Abdallah , Nipashe
Published at 01:03 PM Oct 12 2024
Nembo ya KMKM.
Picha:Mtandao
Nembo ya KMKM.

KMKM SC imepaa kileleni katika msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Mwenge katika mechi ya ligi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Annex B juzi.

Kwa matokeo hayo, KMKM imefikisha pointi 13 wakati Mwenge imesalia kwenye nafasi ya 13 ikijikusanyia pointi nne.

Hiki ni kichapo cha pili mfululizo kwa Mwenge SC ambayo mchezo wake uliopita ilichapwa bila huruma mabao 5-0 na Mafunzo.

Licha ya matokeo hayo, Kocha Msaidizi wa Mwenge, Mustafa Hassan, amesema bado timu yake ina nafasi ya kurekebisha makosa yao na kufanya vizuri katika mechi zinazofuata za ligi hiyo ya juu Zanzibar.

Hassan alisema timu yake imeendelea kupata uzoefu wa michezo ya Ligi Kuu Zanzibar na sasa wameanza kupanga mikakati na kutumia mbinu mpya zitakazowabeba.

Aliongeza bado ugeni wa Ligi Kuu kwa baadhi ya wachezaji wake umekuwa ni tatizo linalowasumbua hasa pale wanapocheza na timu kongwe.

"Ninaamini timu itabadilika, hii inatokana na kiwango wanachokionyesha katika michezo waliyocheza hapa Unguja. Ligi bado changa na bado tunayo nafasi ya kufanya vizuri katika michezo iliyobaki, lengo letu ni kuhakikisha tunakusanya pointi 20 katika mzunguko huu,” kocha huyo alisema.