RC Kunenge ahamasisha uandikishaji kwa mbio za Marathon

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 05:01 PM Oct 12 2024
RC Kunenge ahamasisha uandikishaji kwa mbio za Marathon
Picha:Julieth Mkirire
RC Kunenge ahamasisha uandikishaji kwa mbio za Marathon

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, ameshiriki mbio za marathoni ili kuhamasisha uandikishaji na kujitokeza kushiriki uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

 Mbio hizo zilianza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, zikapita barabara ya Loliondo, na kuhitimishwa katika stendi ya zamani ya Mailimoja, ambapo wananchi zaidi ya 1,000 walihudhuria.

Kunenge alitumia fursa hiyo kuwasihi wananchi kujitokeza kujiandikisha katika daftari la kudumu mapema ili waweze kushiriki uchaguzi na kuwachagua viongozi wanaowataka.

 Ameonya kuhusu hatari ya kusubiri hadi dakika za mwisho ndio watu wajitokeze kujiandikisha, ambapo foleni kubwa inaweza kuwa kikwazo kwa wengine.

"Wastani wa saa moja ni watu sita, hivyo tulijipanga na kuwahi kwenye vituo mapema. Unajiandikisha, kisha unaendelea na shughuli zako za kujiitafutia kipato," amesema Kunenge.

Monica Philemon, mmoja wa wakazi wa Mailimoja, amesema mbio hizo zimeleta hamasa kubwa kwa wananchi na kuwakumbusha wengine ambao walikuwa hawana taarifa kuhusu kuanza kwa uandikishaji. 

George Samson, mfanyabiashara wa eneo hilo, aliongeza kuwa juhudi hizo zinawasaidia wananchi ambao hawana taarifa kuhusu vituo vya uandikishaji na tarehe za mwisho.