Bashe: Tunaondoa ukiritimba vyama vya ushirika vya tumbaku

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:37 PM Oct 12 2024
 Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.
Picha: Mpigapicha
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe.

WATUMISHI wa Vyama vya Ushirika na Taasisi za Fedha wamepewa onyo kali kuacha mara moja kuhujumu malipo ya wakulima wa tumbaku.

Onyo hilo limetolewa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe wakati wa mkutano wa hadhara wa Makamu wa Rais Dk.Philip Mpango katika viwanja vya TASAF, Wilayabya Sikonge mkoani Tabora.

Bashe alisema endapo kutabainika watumishi kuhujumu malipo ya wakulima hatua kali dhidi yao zitachukuliwa.

“Tunasafisha Vyama vya Ushirika.Kwa hiyo kiongozi na mtumishi yeyote atakayebainika kuhusika kwenye ubadhirifu wa fedha za wakulima, atasimamishwa kazi mara moja na hatua nyingine dhidi yake zitachukuliwa,” amesema Bashe.

Bashe amemueleza Makamu wa Rais kuwa wizi wa fedha zaidi ya Sh. milioni 550 umefanywa katika Chama cha Ushirika cha Kisanga ukihusisha watumishi 13 wanaotoka Tume ya Ushirika, TAMISEMI na Benki ya NMB ambapo mtumishi wa Ushirika amesimamishwa kazi.

Baada ya kupewa taarifa ya ubadhilifu wa fedha hizo, Makamu wa Rais ameiagiza TAMISEMI nayo imsimamishe kazi mara moja mtumishi wao aliyetuhumiwa katika kashfa hiyo huku akimtaka Waziri Bashe awasiliane na Meneja Mkuu wa Benki ya NMB ili wawachukukulie hatua watumishi wao wanaotuhumiwa katika hujuma hiyo.

Bashe amesema tayari hatua dhidi ya watuhumiwa hao zimeanza kuchukuliwa  na Mwendesha Mashtaka wa Serikali kwa kushirikiana na TAKUKURU na kwamba Sh. milioni 117 zilizopatikana kutoka kwa watuhumiwa hao na Sh. milioni 437 zimezuiliwa kwenye akaunti zao pamoja na nyumba na magari yao.

Kadhalika, Bashe amesema kampuni ya Voedsel nayo inadaiwa Dola za Marekani 78,000 kwa wakulima wa Chama cha Ushirika cha Mtapenda ambapo hatua zinaendelea kufuatilia ili wakulima walipwe fedha zao. 

“Makamu wa Rais tabia hizo zimesababisha kubadilisha utaratibu wa malipo kwa wakulima,tunataka kwamba  mwanachama halali hta kama hana hisa, ushuru wake uwe ndiyo uhalali wa uanachama wake.  Tunaondoa ukiritimba wa watu kwenye vyama,” amesema Bashe. 

Wilaya ya Sikonge inazalisha sana mazao ya kilimo ambapo uzalishaji wa Tumbaku umeongezeka kutoka tani 10,565 mwaka 2023/24 kutoka tani 2,650 mwaka 2019/2020. 

Uzalishaji wa mazao hayo kwa mwaka 2023/24 ni Dola za Marekani milioni 23.9.