Balozi wa China asema uhusiano wa China na Tanzania unazaa matunda

By Elizabeth John , Nipashe
Published at 05:29 PM Oct 12 2024
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian
Picha:Mpigapicha Wetu
Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian

Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, amesema kuwa uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China unahamasisha ushirikiano katika miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo sekta ya afya.

Katika muktadha huo, amesema kuwa timu ya madaktari wa bingwa 27 imeletwa ili kutoa huduma za kibingwa kwa Watanzania.

Mingjian ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kliniki ya kibingwa, ambayo inaendeshwa na serikali ya Tanzania kwa ushirikiano na Ubalozi wa China, katika viwanja vya stendi ya zamani mjini Njombe.

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Athony Mtaka, amesisitiza umuhimu wa wananchi kujenga utaratibu wa kuchunguza afya zao na kupata tiba. “Tupo na madaktari bingwa, madaktari bobezi na vifaa. Hivyo, kama una mgonjwa nyumbani, ni vyema kutumia fursa hii,” amesema Mtaka.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Juma Mfanga, ameongeza kuwa ubalozi wa China umeleta matibabu ya kibingwa ambayo yatatolewa bure.