Simba, Yanga mtegoni CAF

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 10:19 AM Oct 08 2024
Simba, Yanga mtegoni CAF
Picha:Mtandao
Simba, Yanga mtegoni CAF

WAKATI Mabingwa wa Tanzania Bara wakipangwa Kundi A kwenye hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Al Hilal ya Sudan na MC Alger ya Algeria, wawakilishi wa nchi kwenye Kombe la Shirikisho, Simba nao wamepangwa Kundi A, likitajwa kuwa ni kundi la kifo.

Simba inatarajiwa kuanzia nyumbani dhidi ya Bravo do Maquis ya Angola, Novemba 28, kama ilivyo kwa Yanga ambayo nayo itaikaribisha Al Hilal kati ya Novemba 26-27, mwaka huu.

Makamu Rais wa Klabu ya Yanga, Haji Arafat, amesema hakuna timu rahisi katika kundi lao, bali ubora wa vikosi ndivyo vitakavyoamua, huku lengo lao likiwa ni kivuka hatua ambayo waliishia msimu uliopita.

Kwa mujibu wa droo iliyopangwa jana Makao Makuu ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), jijini Cairo, Misri, Simba iko kundi moja na timu za CS Costantine ya Algeria, na CS Sfaxien ya Tunisia.

CAF, imelitaja kundi hilo kuwa la kifo kutokana na ubora wa timu zilizoko, ikiwamo Simba yenyewe ambayo imekuwa ikifanya vema kwenye michuano ya kimataifa.

Klabu ya CS Sfaxien, ambayo imelitwaa Kombe la Shirikisho Afrika mara tatu, 2007, 2008 na 2013, ikiwahi pia kulitwaa 1998 wakati likiitwa Kombe la CAF, ambapo Simba ilifika fainali 1993.

Timu hiyo ilifika fainali ya Kombe la Shirikisho 2010, lakini pia ilicheza fainali tatu za Super Cup, inayochezwa dhidi ya Mabingwa wa Afrika na Kombe la Shirikisho, 2007, 2009 na 2014 na kupoteza.

CS Sfaxien ilifika nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1996 na 2006, huku ikifika fainali 2014.

Yanga itakutana tena na timu tatu ambazo zimeshawahi kukutana nazo kwenye hekaheka za michuano hiyo.

Itacheza na MC Alger ambayo ilikutana nayo kwenye hatua ya makundi, Kombe la Shirikisho, Aprili 8, 2017, ikishinda bao 1-0 nchini na kwenda kupoteza kwa mabao 4-0 ugenini, Aprili 15, 2017.

Kwa mara nyingine tena itavaana uso kwa uso na TP Mazembe ambayo msimu 2022/23, ilikutana nayo kwenye hatua ya makundi Kombe la Shirikisho, ikishinda mabao 3-1, Februari 19, 2023 nchini na kwenda kushinda tena ugenini nchini DR Congo bao 1-0.

Kwenye kundi hilo pia kuna Al Hilal ambayo iliinyima Yanga nafasi ya kwenda hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika 2022/23, na badala yake kuangukia Kombe la Shirikisho.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, Oktoba 8, 2022, mchezo ukipigwa hapa nchini, na Yanga kuchapwa bao 1-0 katika mchezo wa marudiano nchini Sudan, uliochezwa Oktoba 16, 2022.

Hata hivyo, kwa mujibu wa CAF, kwenye Ligi ya Mabingwa, Mabingwa Watetezi, Al Ahly, iliyopo Kundi C sambamba na CR Belouizdad ya Algeria, Orlando Pirates (Afrika Kusini) na Stade d’Abidjan ya Ivory Coast, ndilo linaloelezwa kuwa gumu zaidi.

"Hatua hii hakuna timu rahisi, timu zote ambazo zimeingia kwenye hatua hii ni ngumu na zina malengo ya kufika mbali, TP Mazembe tuliwafunga nje na ndani kwenye Kombe la Shirikisho, lakini mwaka huu wameboresha kikosi chao, Al Hilal nao pia tumeshawahi kukutana nao, ni timu ambayo imeendelea kulinda kiwango chao, iko vile vile, haijaporomoka kiwango pamoja na kwamba nchini kwao kuna matatizo ya vita na hawana ligi nyumbani, si timu ya kubeza ni timu iliyojipanga tuliona ilipokuja kucheza hapa na Algeria tumeshakwenda mara kadhaa tunazifahamu timu za huko," alisema Arafat.

Pamoja na hayo alisema wao wanajipanga kuipeperusha vizuri bendera ya Tanzania akiwataka mashabiki kujazana kwa wingi viwanjani wakati timu hiyo ikicheza.

"Uzuri ni kwamba sisi kama Yanga tuna kikosi kizuri, bora na tumejipanga kuhakikisha timu yetu inafanya vizuri msimu huu, wachezaji wetu walikuwa hapa, wameona jinsi viongozi wao na mashabiki wao walivyokuwa na hamasa wakati wa upangaji wa droo," alisema.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally, alisema wamefurahi kucheza na timu ambazo hawajawahi hata siku moja kukutana nazo kwenye michuano ya Afrika.

"Tumefurahi aina ya wapinzani ambao tumepangiwa, kwanza kwetu ni wapinzani wapya hatujawahi kukutana kwenye pilikapilika zetu kwenye michuano ya makombe ya Afrika, tutakwenda kucheza Algeria, tutakwenda kucheza Tunisia nchi ambayo kwa miaka ya karibuni hatujawahi kwenda kucheza mechi yoyote ile, kwa hiyo msimu huu tunakwenda kucheza tukiwa na wapinzani wapya kabisa.

"Angola tuliwahi kwenda kucheza na Primeiro de Agosto, Algeria tulikwenda kucheza na Mo Bejaia," alisema Ahmed ambaye amesema wamejiandaa kukabiliana na timu hizo.

Timu za Tanzania zote zitaanzia nyumbani, Yanga ikianza Novemba 26 au 27 dhidi ya Al Hilal Ligi ya Mabingwa, Simba ikikipiga Novemba 28 dhidi ya Bravo do Maquis.

Pia zitamalizia mechi zao nyumbani, Yanga ikicheza dhidi ya MC Alger, Januari 17 au 18, kabla ya Simba kushuka Januari 19, mwakani dhidi ya CS Costantine ya Algeria.

 

MAKUNDI YOTE LIGI YA MABINGWA

KUNDI A

TP Mazembe (DR Congo)

Yanga (Tanzania)

Al Hilal (Sudan)

MC Alger (Algeria)

 

KUNDI B

Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)

Raja Casablanca (Morocco)

AS FAR (Morocco)

Maniema Union (DR Congo)

 

KUNDI C

Al Ahly (Misri)

CR Belouizdad (Algeria)

Orlando Pirates (Afrika Kusini)

Stade d’Abidjan (Ivory Coast)

 

KUNDI D

Esperance (Tunisia)

Pyramids FC (Misri)

Sagrada Esperanca (Angola)

Djoliba (Mali)

 

MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO

 

KUNDI A

Simba SC (Tanzania)

CS Sfaxien (Tunisia) 

CS Constantine (Algeria)

FC Bravos do Maquis (Angola)

 

KUNDI B

RS Berkane (Morocco)

Stade Malien (Mali)

 Stellenbosch (Afrika Kusini) 

CD Lundal Sul (Angola)

 

KUNDI C

USM Alger (Aligeria)

ASEC Mimosas (Ivory Coast)

ASC Jaraaf (Senegal)

Orapa United (Botswana)

 

KUNDI D

Zamalek SC (Misri)

Al Masry (Misri)

Enyimba (Nigeria)

Black Bulls (Msumbiji)