Mgoyi achaguliwa kuiongoza Kigoma

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:08 AM Sep 21 2024
AHMED Mgoyi
Picha: Mtandao
AHMED Mgoyi

AHMED Mgoyi amechaguliwa tena kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Kigoma (KFA), katika uhaguzi mkuu uliofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Lake Tanganyika jana.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya KFA, Wakili Sadiki Aliki, alisema Mgoyi ameibuka mshjndi baada ya kupata kura zote za ndio.

Aliki alimtangaza Mbuya Kilima amekuwa Makamu Mwenyekiti baada ya kupitishwa na wajumbe wa Mkutano Mkui wa KFA huku Issa Bukuku akichaguliwa kuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Shirikisho cha Soka Tanzania (TFF).

Aliwatangaza waliochaguliwa kuwa wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni pamoja na Issaya Manega na Denissa Buberwa.

Wakati huo huo Mgeni rasmi katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao, aliwapongeza KFA kwa kufanya mashindano mbalimbali na kuahidi shirikisho litaendelea kuwaunga mkono katika shughuli zote za maendeleo ya mpira wa miguu.

Kidao kwa upekee alitangaza kuipatia wilaya ya Kakonko mipira 50 kutokana na juhudi zao za kusimamia na kuendesha mashindano mbalimbali ambayo yameongeza hamasa mkoani humo.

Alisema pia TFF imepanga kuwekeza katika miundomimbu mkoani humo na itaanza na kujenga uwanja bora kwa ajili ya mashindano ya soka la ufukweni.