Kocha: Hii ndiyo Azam ninayoitaka

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:05 AM Sep 21 2024
Kocha Mkuu wa Azam FC Rachid Taoussi
Picha:Mtandao
Kocha Mkuu wa Azam FC Rachid Taoussi

KOCHA Mkuu wa Azam FC Rachid Taoussi, ameonesha kuridhishwa na kiwango cha wachezaji wake walichokionesha juzi jioni kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam, ilipoisasambua KMC mabao 4-0, akisema hicho ndicho kiwango alichokuwa akikihitaji.

Raia huyo wa Morocco, mara baada ya mchezo huo, alisema katika mchezo dhidi ya Pamba Jiji ambao uliisha kwa suluhu, alibainisha timu yake kucheza vyema lakini wanashindwa kufunga mabao, lakini juzi alicheza vizuri na kupachika mabao, kitu kinachoonesha kuwa mafunzo yanawaingia vizuri wachezaji wake.

"Ndicho tulichokuwa tunahitaji, nilisema wakati mwingine unaweza ukacheza vyema lakini usipate mabao kama tulivyofanya katika mchezo dhidi ya Pamba, lakini unaweza ukacheza vibaya ukapata mabao, na unacheza vizuri ukapata mabao vile vile, leo tumecheza vizuri na kupata mabao mengi, hivi ndivyo ninavyohitaji na nahitaji muendelezo katika hili," alisema kocha huyo.

Yalikuwa ni mabao ya Idd Suleiman 'Nado', akiwa ndiye mchezaji wa kwanza wa Azam kupachika bao msimu huu, akifunga dakika ya 19, Lusajo Mwaikenda, dakika ya 55, Nassor Saadun dakika ya 60 na Fredy Tangalo wa KMC alijifunga katika harakati za kuokoa.

Kwa upande wa  kocha wa KMC, Abdihamid Moallin alisema wamefungwa mabao yote hayo kutokana na kufanya makosa mengi upande wa ulinzi.

"Tumefanya makosa mengi ya kiulinzi, lakini hatuwezi kuendelea kulia, badala yake tukakwenda kwenye uwanja wa mazoezi kuangalia nini tutafanya kwenye mchezo wetu unaofuata dhidi ya JKT Tanzania," alisema kocha huyo raia wa Somalia.

Kwa matokeo haya, Azam inapanda kuyoka nafasi ya 10 hadi ya sita, ikiwa na pointi tano, ukiwa ni ushindi wao wa kwanza baada ya kusuluhu mbili, huku KMC, ikiwa kwenye nafasi ya nane na pointi zake nne.