Gamondi: Tumejiandaa kuingia makundi kwa kishindo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:45 AM Sep 21 2024
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.
Picha:Mtandao
Kocha wa Yanga, Miguel Gamondi.

KOCHA wa Yanga, Miguel Gamondi, amesema wamejipanga kuhakikisha wanatinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kishindo kwenye mchezo wa leo wa marudiano raundi ya kwanza dhidi ya CBE ya Ethiopia.

Kwenye mchezo wa leo, Yanga inahitaji sare au ushindi wa aina yoyote kuweza kusonga mbele kufuatia ushindi wa bao 1-0 walioupata ugenini kwenye mchezo wa kwanza.

Akizungumza mjini hapa jana, Gamondi, alisema wamejiandaa vizuri na wapo tayari kwa ajili ya mchezo huo ingawa ameutabiri utakuwa mchezo mgumu na wenye upinzani.

Alisema anataka kuona kile alichokifanyia kazi mazoezini kinamletea matokeo chanya kwenye mchezo wake na amewataka wachezaji wake kuhakikisha wanatumia vizuri kila nafasi wanayoipata kwenye mchezo huo.

"Nimekuwa nikifanyia kazi tatizo la kukosa magoli, kwa siku za karibuni tunatengeneza nafasi nyingi lakini hatuzitumii na kujikuta kama tunashinda tunashinda kwa magoli machache, naamini kwenye mchezo wa kesho hali haitakuwa hivyo, tunataka kuona tunatinga hatua ya makundi kwa kishindo," alisema Gamondi.

Pamoja na hayo, Gamondi amesema hataki wachezaji wawe na presha kwa kuwa tayari watanguliza mguu mmoja na wanachotakiwa ni kuwa na utulivu na kucheza soka lao la kila siku akiwasisitiza zaidi kutumia vizuri nafasi.

"Wapinzani wetu hawana cha kupoteza, wapo nyuma kwa bao moja hivyo watakuja kwa kasi na kutaka kutushambulia kuweza kusawazisha bao tulilowafunga, nimewataka wachezaji wangu kuwa makini nao na kucheza kwa tahadhari licha ya kuwa  tupo nyumbani," alisema Gamondi.

Wakizungumza juu ya mchezo huo, nyota wa Yanga, Dikson Job na Ibrahim Baka, wamesema wanajiandaa vizuri na mchezo huo na wapo tayari kuhakikisha wanaipeleka Yanga hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili ndani ya kipindi cha miaka miwili.

"Yapo makosa madogo madogo ambayo yalionekana kwenye mchezo uliopita, benchi letu la ufundi limefanyia kazi na tupo tayari sasa kwa mchezo huu," alisema Job.

"Tunaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti, tunaamini hatutawaangusha, mashabiki wamekuwa wakitusapoti sana na hii ni nafasi nyingine ya kuwashukuru kwa kuhakikisha tunapata ushindi mzuri," alisema Bacca.

Kwa upande wake, Kocha wa CBE, Leulelsegd Betsalot, alisema mchezo utakuwa mgumu kwa kuwa wanacheza na timu kubwa na yenye uzoefu wa kutosha lakini watajaribu kucheza kwa utulivu na akili kubwa.

"Dakika 90 ndizo zitakazoamua, Yanga ni timu kubwa na kwetu tunaona tuna mlima mkubwa wa kuupanda kuweza kuwatoa, lakini kwenye mpira lolote linawezekana, tutapambana kwa akili kubwa kujaribu kuwarudisha nyuma na ikiwezekana kupata ushindi," alisema Betsalot.

Endapo Yanga watafanikiwa kuwatupa nje CBE, watakuwa wamefuzu hatua ya makundi ya michuano hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya mwaka jana kufika mpaka hatua ya robo fainali na kutolewa kwa mikwaju ya penalti ya Mamelod Soundowns.