Benchikha atoa sababu kuvunja mkataba Simba

By Adam Fungamwango ,, Saada Akida , Nipashe
Published at 08:26 AM Apr 29 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, Kamal Boujnane na Farid Zemit, katika picha wakati wakitambulishwa walipojiunga na klabu hiyo kabla ya jana kuachana na klabu hiyo.
Picha: Maktaba
Kocha Mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha, Kamal Boujnane na Farid Zemit, katika picha wakati wakitambulishwa walipojiunga na klabu hiyo kabla ya jana kuachana na klabu hiyo.

HATIMAYE ni rasmi sasa Klabu ya Simba, imefikia makubaliano ya pande zote mbili ya kuvunja mkataba kati yake na Kocha Mkuu, Abdelhak Benchikha pamoja na wasaidizi wake wawili Kamal Boujnane na Farid Zemit.

Awali, baada ya kutwaa Kombe la Muungano juzi visiwani Zanzibar kwa kuifunga Azam FC bao 1-0 kwenye mchezo wa fainali uliopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, zilizuka taarifa za chini kwa chini kuwa kocha huyo ameomba kuvunja mkataba kutokana na kile kilichodaiwa kuwa haioni Simba ikimfanya kupata mafanikio ya kutwaa makombe makubwa barani Afrika.

Simba ilishindwa kufuzu hatua ya nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikiwa chini yake, kisha kutolewa kwenye Kombe la FA maarufu CRDB Bank Confederation Cup huku pia ikiwa na nafasi finyu ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara, mataji hayo mawili ndiyo yanayotoa nafasi kwa klabu kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao. 

Taarifa zaidi zilidai kuwa Benchikha anamini kuwa Simba haina wachezaji bora ambao wanaweza kutimiza ndoto zake hizo.

Hata hivyo, akizungumza na Nipashe jana, Meneja Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally, alisema Mwalimu Benchikha ameomba kuvunja mkataba wake kutokana na matatizo ya kifamilia yanayomkabili nyumbani kwao Algeria.

Alisema Benchikha ameueleza uongozi wa Simba kuwa anauguliwa na mkewe, hivyo anahitaji muda kuwa karibu naye na kumuuguza, kwa namna hiyo kwa kuzingatia umuhimu wa jambo hilo uongozi umeridhia ombi la kocha huyo.

"Uongozi wa Klabu ya Simba unamshukuru Mwalimu Abdelhak Benchikha kwa kipindi chote  alichotumia ndani ya timu yetu na tunamtakia kila la heri na tunamuombea mkewe apate afya njema," alisema Ahmed.

Wakati huo huo, uongozi wa klabu hiyo umemteua Mwalimu Juma Mgunda kukiongoza kikosi hicho akisaidiwa na Selemani Matola hadi hapo Bodi ya Wakurugenzi itakapotoa uamuzi mwingine.

Mwalimu Juma Mgunda ataanza kazi katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya Namungo FC utakaochezwa kesho, Jumanne  Ruangwa Mkaoni Lindi katika Uwanja wa Majaliwa saa 12 jioni.

Katika hatua nyingine, baada ya Simba kutwaa ubingwa wa Muungano, wachezaji wa timu hiyo wamesema wameamua kuutoa kwa mashabiki wao, wakisema utakuwa chachu ili baadhi yao waliokata tamaa warejee kuwasapoti, huku wao wakiendelea kupigania nembo ya klabu hiyo.

Wakizungumza baada ya kumalizika kwa mechi ya fainali ya Muungano, Uwanja wa New Amani Complex, Zanzibar, juzi, Simba ikipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Azam FC, likiwekwa wavuni na kiungo mkabaji raia wa Senegal, Babacar Sarr, wachezaji hao wamesema ubingwa walioupata unakwenda kwa mashabiki wao ambao siku za karibuni wamekuwa hawana furaha kutokana na timu yao kutofanya vema, huku wakiwataka sasa kurejea na kujaza viwanja kama ilivyokuwa zamani.

"Kiukweli tumefurahishwa na matokeo ya leo, na tumecheza leo kwa ajili ya kuwapa furaha mashabiki wetu, yaani tumecheza kwa ajili ya mashabiki wenye Simba yao, na ubingwa huu ni wao,  tunawaambia kuwa bado tunaweza, tunapambania furaha yao na kwa ajili ya nembo ya klabu.

Tunarudi kwenye ligi, kikubwa baada ya kombe hili, nadhani mashabiki watakuwa na imani na sisi, watarejea kwa wingi viwanjani ili kutupa sapoti, wasituache, sisi ndiyo wachezaji wao mpaka mwisho wa msimu, tumejipanga vizuri tutahakikisha mechi zote zilizobaki tunashinda," alisema Kibu Denis.

Kiungo mkabaji, Mzamiru Yassin alisema wao kama wachezaji walicheza kwa ajili ya kulitwaa kombe hilo ili kurudisha imani kwa mashabiki na kweli wamefanya hivyo, huku akiwaangukia kuwa ubingwa huo sasa uwafanye waje viwanjani kuwapa sapoti kama zamani na wao watahakikisha kuwa wanawapa furaha.

Kwa upande wa Saido Ntibazonkiza yeye aliwashukuru mashabiki waliojazana uwanjani kuwashangilia, akisema shabiki wa kweli hawezi kuiacha timu yake

"Huu ni mpira, shabiki wa kweli hawezi kuiacha timu yake, hawa waliopo hapa wanaotushangilia na wanaoendelea kutupa sapoti ndiyo mashabiki wa kweli, katika soka huwezi kushinda kila siku, hata timu kubwa huwa zinapoteza," alisema.

Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Mohamed Hussein 'Tshabalala', alisema ubingwa walioupata ni chachu ya kufanya vema kwenye mechi zilizosalia za Ligi Kuu.

Ushindi huo unaifanya Simba kuwa bingwa wa kombe hilo mara sita sawa na Yanga, ambapo kwa sasa zote zinaongoza kwa kutwaa mara nyingi zaidi.

Simba ilifanya hivyo mwaka 1993, 1994, 1995, 2001 na 2002, kabla ya kutwaa tena juzi, huku Yanga ikilichukua 1983, 1987, 1991, 1996, 1997 na 2000.