ACT-Wazalendo wataka uchunguzi kutekwa kijana Sativa

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 04:00 PM Jun 27 2024
kijana Edgar Mwakabela, maarufu kama Sativa.
Picha: Mtandao
kijana Edgar Mwakabela, maarufu kama Sativa.

CHAMA cha ACT-Wazalendo kimetaka kufanyike uchunguzi kuhusiana na tukio la kutekwa, kuteswa na kujeruhiwa kwa kijana Edgar Mwakabela, maarufu kama Sativa, mkazi wa mbezi, Dar es Salaam.

Hivi karibuni kulikuwa na taarifa iliyokuwa ikisambaa kwenye mitandao ya kijamii ya kupotea kwa kijana huyo tangu Juni 23 mwaka huu ambaye leo amepatikana mkoani Katavi akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.

“Watanzania wameanza kuingiwa tena na hofu kukithiri kwa matukio ya wananchi kupotea, kuteswa na kuuawa kwa kasi siku za hivi karibu. Tunalaani kwa nguvu zote kuongezeka kwa matukio hayo bila hatua madhubuti kuchukuliwa,”amesema Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dahlia Majid.

Amesema chama hicho kimejitolea kumrejesha Dar es Salaam kwa ndege kijana huyo ili apatiwe matibabu ya haraka.

“ACT Wazando tumechukua hatua za kumrejesha Dar es Salaam kwa Ndege kijana Mwakabela ili apatiwe  matibabu haraka na ya kibingwa. Hata hivyo, tunataka hatua za haraka za uchuhguzi zifanyike ili kubaini watu waliohusika na utekaji wake,”amesema Majid.