Serikali kuweka mkazo kuondoa vijana kwenye uraibu wa dawa za kulevya

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:30 PM Jun 29 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama akiwakabidhi cheti cha Ushiriki Jeshi la Uhamiaji katika  Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Dunia 2024 yanayofanyika Jijini Mwanza.
Picha: Mpigapicha Weru
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama akiwakabidhi cheti cha Ushiriki Jeshi la Uhamiaji katika Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Dunia 2024 yanayofanyika Jijini Mwanza.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama amesema Serikali inaendelea kuweka nguvu katika kuondoa vijana kwenye uraibu wa dawa za kulevya kwa kuhakikisha inawapa tiba vijana hao ili warudi katika hali zao za kawaida.

Kauli hiyo ameitoa leo Juni 29, 2024 wakati alipotembelea Mabanda ya Taasisi mbalimbali kuelekea Maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Dunia 2024 zinazofanyika Jijini Mwanza katika Uwanja wa Nyamagana.

"Tumeshuhudia vijana wengi waliotoka kwenye uraibu wa dawa za kulevya wamerudi kuwa rai wazuri wanajishughulisha na shughuli za uzalishaji mali na wameamua kujitokea kuokoa vijana wenzao," amesema Waziri Mhagama

Waziri Mhagama amefafanua kwamba, “Serikali imeshajenga kituo Jijini Dodoma cha urekebishaji ambacho kitakuwa kinatoa tiba ya kutoa vijana kwenye uraibu wa dawa za kulevya na kufundisha mafunzo ya ujuzi."

Aidha Serikali imeleendelea kutekeleza kwa nguvu kubwa kwenye matamko ya kisera ili kuweza kuhakikisha inaokoa vijana kwenye matumizi ya dawa za kulevya.

"...pia tunaamini Serikali kwa kushirikiana na wadau wengine tukifanya kwa pamoja tunaweza kupata mafanikio makubwa sana," amesema

Waziri Mhagama amesema pia kwa tafiti zilizofanyika mtumiaji akitumia dawa za kulevya anatumia masaa sita kwa kilevi ambacho kinamsababishia kulala na kutojitambua masaa sita, jambo ambalo linamnyima uwezo wa kufanya kazi, anapopata fahamu anakuwa dhaifu na hawezi ufanya kazi yoyote na anapokosa fedha ya kununua madawa inamsababisha kuingia kwenye matendo ya jinai.

Awali Katika zoezi hilo Waziri Mhagama aliambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy Nderiananga pamoja na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera Bunge na Uratibu Dk. Jim Yonazi.