MASHAMBULIZI M23; Tanzania yapoteza askari wawili, wanne wajeruhiwa

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 01:22 PM Feb 02 2025
Kaimu Mkurugenwa Habari na Uhusiano JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda
Picha: Mtandao
Kaimu Mkurugenwa Habari na Uhusiano JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda

JESHI la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), limesema limewapoteza askari wake wawili na wengine wanne kujeruhiwa, kufuatia mashambulizi ya mfululizo katika maeneo ya Sake na Goma, yaliyofanywa na waasi wa M23, Januari 24 na 28, mwaka huu.

Kaimu Mkurugenwa Habari na Uhusiano JWTZ, Kanali Gaudentius Ilonda, amesema hayo leo, na kwamba majeruhi wanaendelea kupatiwa matibabu mjini Goma.

Amesema jeshi hilo limekuwa likishiriki shughuli za Ulinzi wa Amani chini ya Mwamvuli wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya za Kikanda ikiwemo Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

“Taratibu za kuisafirisha miili ya marehemu pamoja na majeruhi waliotokana na mapigano hayo zinaendelea kupitia Sekretarieti ya SADC. 

“Mwenyezi Mungu awape uponyaji wa haraka majeruhi wetu na aziweke Roho za Marehemu Mahali Pema Peponi, Amina.

“Aidha, vikundi vyetu villivyopo nchini DRC vipo salama, imara na vinaendelea kutekeleza majukumu yake kwa maelekezo ya Uongozi wa SADC,” amesema.