HOJA ZA WAWEKEZAJI; Serikali yawaita mabalozi watete

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:28 AM Jun 29 2024
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.
Picha: Mtandao
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba.

MABALOZI 10 nchini wameomba mkutano wa dharura na mawaziri watatu wa Tanzania kwa lengo la kutatua changamoto za uwekezaji zilizojitokeza, serikali imewakubalia.

Hao ni pamoja na Michael Battle anayewakilisha Marekani nchini, David Concar (Uingereza), Wiebe de Boer (Uholanzi), Nabil Hajlaoui (Ufaransa), Peter Hughebaert (Ubelgiji), Kyle Nunas (Canada) na Charlotta Macias (Sweden).

Wengine ni Thomas Terstegen (Ujerumani), Seungyun Lee (Korea) na Mags Gaynor anayewakilisha Ireland nchini.

Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January Makamba, imeahidi kuzifanyia kazi kwa haraka changamoto zinazokumba wawekezaji wa kigeni nchini ambazo zimeainishwa na mabalozi hao.

Miongoni mwa mambo waliyotaja mabalozi hao kupitia barua yao ya pamoja ya Juni 26 mwaka huu, ni wasiwasi kuhusu utaratibu wa usimamizi wa kodi unaofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa wawekezaji wa kigeni, wakitaka serikali kuingilia kati.

Katika barua yao hiyo, mabalozi wameomba kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki mwenyewe, Waziri wa Fedha, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais -Uwekezaji na Mipango, Waziri wa Viwanda na Biashara na Kamishna Mkuu wa TRA ili kujadili namna ya kutatua vikwazo vinavyolalamikiwa na wawekezaji kutoka mataifa yao.

Akijibu barua yao juzi, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, January, amekubali kuzungumza nao, akisema serikali inaheshimu utawala bora na wa kisheria kama nguzo muhimu za maendeleo na ustawi.

"Tunajivunia kuwa na utawala wa kisiasa na kiuchumi ambao unavutia uwekezaji na kuwezesha maendeleo ya sekta binafsi.

"Ili mkutano huo uwe na tija, ninaomba wawekezaji unaowarejelea waandae muhtasari/uwasilishaji unaoelezea kwa uwazi, malalamiko yao," alisema Waziri January akimjibu Balozi wa Ufaransa nchini, Nabil Hajlaoui, aliyeandika barua hiyo kwa niaba ya mabalozi wenzake.

Waziri huyo alisema mafanikio ya kuvutia uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) ndani ya Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, yanathibitisha imani ambayo jumuiya ya kimataifa ya uwekezaji inayo kwa Tanzania.

"Ningependa kuwahakikishia kuwa serikali hii inachukua kwa uzito mkubwa ukiukwaji wowote unaodaiwa kufanywa na taasisi yoyote ya umma, ambayo inahatarisha mafanikio ya biashara yoyote katika nchi yetu na sifa yetu kama kivutio rafiki kwa wawekezaji," alisema January.

YALIYOMO

Katika barua yao ya Juni 26 mwaka huu, mabalozi hao wanashauri serikali kuzingatia umuhimu wa kujibu mapema suala hilo la dharura kama walivyoomba.

Wanasema mafanikio makubwa katika kuvutia na kupanua uwekezaji wenye ubora wa kimataifa nchini katika kipidi cha miaka michache iliyopita yanakabiliwa na usumbufu mkubwa kutokana na notisi zisizo na ushahidi kutoka TRA zinazodai malipo na masuluhisho ya akaunti yaliyowataka walipe madai hadi ya miaka 15 iliyopita.

Kwa mujibu wa mabalozi hao, usajili wa uwekezaji wa biashara uliongezeka kutoka Dola za Marekani bilioni tatu mwaka 2022 hadi Dola za Marekani bilioni 5.5 mwaka 2023, jambo linaloonesha ushirikiano mzuri kati yao na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

"Wawekezaji pia wanaripoti kuwa mawakala wa TRA hutoza bili zisizo za kawaida za kodi zisizoungwa mkono na sheria za Tanzania, hivyo kutishia wawekezaji na washirika wa Tanzania. 

"Pale kampuni zinapopinga au kukata rufani dhidi ya vitendo hivyo, zinatishiwa kufungiwa au kukamata akaunti za benki na mali za kampuni," mabalozi hao wanadai katika barua yao hiyo.

Mabalozi hao wanasema wameendelea kujizatiti kufanya kazi kwa ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika kutafuta suluhu za changamoto hizo zinazokwenda sambamba na kujenga upya imani katika mazingira ya biashara ya Tanzania, sambamba na azma ya nchi kufikia ukuaji uchumi jumuishi na kuwa miongoni mwa nchi zenye kipato cha kati.