Mahakama yaamuru kampuni uchimbaji kuilipa familia mil. 150/-

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:49 AM Jul 01 2024
Kampuni ya Barrick Gold.
Picha:Mtandao
Kampuni ya Barrick Gold.

MAHAKAMA ya Rufani imeamuru kampuni ya Barrick Gold inayojihusisha na uchimbaji madini katika mgodi wa North Mara, wilayani Tarime kulipa familia moja Sh. milioni 150 kwa madhara waliyopata kutokana na shughuli za mgodi huo.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya rufani ya kampuni hiyo kupinga uamuzi wa kesi ya awali iliyofunguliwa katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Mwanza iliyotolewa uamuzi Agosti 3, 2016.

Katika kesi hiyo, Chacha Kiguha, mkewe Neema Chacha na watoto wao, Bhoke Chacha, Kiguha Chacha, Montogori Chacha na Surati Chacha walimshtaki mrufani, Meneja Mkuu, African Barrick Gold Mine Ltd, wakidai malipo ya uharibifu wa jumla wa Sh. 600,000,000.00.

Madai hayo yalitokana na uzembe wa kampuni hiyo kutenda kinyume na wajibu wa kutunza maslahi ya mlalamikaji wakati inamiliki leseni Maalum ya Uchimbaji madini (SML) katika vijiji vitano wilayani hapa kikiwamo kijiji cha wahojiwa cha Nyamwaga na kuwasababishia magonjwa.

Ilidaiwa kwamba familia hiyo ililazimika kuishi katika kipande hicho cha ardhi na kushindwa kuondoka kwa sababu ya mrufani kushindwa kulipa fidia ya haki kwa ajili ya ardhi iliyoathirika. 

"Kitendo cha mshtakiwa kimesababisha kuumia kwa walalamikaji kwa idadi ya miaka kadhaa wamekuwa wakifuatilia fidia zao kwa ofisa wa mshtakiwa na kusababisha mfadhaiko mkubwa wa kiakili na uchungu," ilisema sehemu ya uamuzi huo wa awali.

Mrufani alipinga madai ya walalamikiwa Mahakama ya Rufani huku akikanusha kwamba kampuni hiyo ilishindwa kuzingatia jukumu la uangalizi na hivyo kusababisha wahojiwa kupata maradhi mbalimbali au ugonjwa wa akili kama inavyodaiwa.

Awali kampuni hiyo ilipinga hukumu ya Mahakama Kuu kwa madai, kupitia vitendo vyake vya uchimbaji walalamikaji waliathiriwa kiafya kwa kuambukizwa magonjwa ya kupumua, masikio na ngozi.

Matokeo hayo ya rufani yalitolewa mbele ya Faustine Malongo na Caroline Kivuyo ambao ni mawakili wakati mrufani na mlalamikiwa waliunganishwa kupitia mfumo wa kidijitali wa mahakama unaofahamika kama ‘teleconferencing’.

Baada ya kupitia hoja zote za mrufani kwa niaba ya kampuni hiyo kuhusu hukumu iliyotolewa awali, majaji wa mahakama ya rufani wamekubaliana baadhi huku wakipinga nyingine kwa kukosekana uthibitisho.

Kutokana na uamuzi wa majaji, mjini Musoma mrufani atawajibika kulipa fidia wahojiwa kwa kusababisha kero kwao kutokana na ukiukwaji wa sheria na wajibu wa utunzaji unaosababisha j uharibifu.

"Kuzingatia asili ya uharibifu kwa mlalamikiwa na familia yake, wakiwamo watoto wadogo na ukubwa wa uzembe, mhojiwa anapaswa kupata fidia ya Sh. 25,000,000.00 kwa kila mmoja.

Mlalamikaji anaamriwa kulipa Sh. 150,000,000 pamoja na riba kwa kiwango cha mahakama cha asilimia saba kwa mwaka.

"Katika mazingira ya kesi ambapo uzembe wa kuchangia ni wanaohusika, tunaagiza kwamba kila upande ubebe gharama zake," ilieleza sehemu ya hukumu hiyo iliyotolewa Juni 14, 2024.