Upandikizaji mimba rasmi Muhimbili

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 11:08 AM Jul 03 2024
news
Picha: Christina Mwakangale
Dk. Lisa Rusibamanyila (kushoto) kutoka Idara ya Magonjwa ya Dharura na Maafa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), akifafanua jambo kwa mmoja wa watu waliotembelea Banda la MNH, katika Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa.

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) itaanza rasmi upandikizaji mimba (IVF) Septemba mwaka huu, huku gharama kwa huduma hiyo ikiwa ni Sh. milioni 20.

Bingwa wa Masuala ya Kinamama Kitengo cha IVF MNH (Obstetrician and gynaecologist), Dk. Sabria Rashid, aliyasema hayo jana alipozungumza na Nipashe kwenye banda la hospitali hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya 48 Dar es Salaam (DITF). 

Alisema kuwa kwenye maonesho hayo, kitengo hicho kimekuja na elimu kwa umma kuhusu huduma hiyo ambayo itaanza miezi miwili ijayo.

Bingwa huyo alisema kuwa wataanza na kundi la watu 10 kupewa huduma, akieleza kuwa gharama za upandikizaji ni kubwa kutokana na mahitaji ya dawa na vifaa ambavyo bei yake ni ghali. 

"Mahitaji ya IVF ni makubwa. Tumewaona kliniki na wapo katika mchakato. Tukianza mwezi wa tisa (Septemba), tutaanza na hao ambao tutawasiliana nao. Unapozungumzia IVF siyo mwanamke tu, wapo wanaume ambao ni chanzo cha ugumba. 

"Tukifanya uchunguzi na kugundua tatizo ni la baba, tutapandikiza mimba kwa mwanamke, lakini mbegu ya kiume kuchukuliwa pengine kwa mwanamume ambaye mbegu yake ni dhaifu. Jamii ijue utasa ni kwa jinsi zote," alisisitiza Dk. Sabria. 

Bingwa huyo alisema wanaotafsiriwa kwamba ni wagumba ni walio kwenye uhusiano ama wanandoa waliopo pamoja kwa takribani mwaka mmoja na hushiriki tendo bila kufanikisha lengo lao la kupata mtoto. 

Alisema ugumba upo wa aina mbili; waliopata mtoto na kukaa miaka kadhaa wakitafuta mtoto mwingine na ambao tangu kuzaliwa hawajawahi kushika ujauzito. 

"Umri ukienda ni tatizo. Lakini tunapata pia walio katika umri wa kati. Kwa sasa kutokana na sababu za kimazingira, mabadiliko ya mtindo wa maisha kama vile watu wanatafuta elimu kwanza, kisha watoto. 

"Utakuta umri unakwenda, kuja kuanza kutafuta mtoto tayari changamoto. Pia wapo vijana wadogo wameathiriwa na mazingira tofauti na zamani wenye umri mdogo hawakupata tatizo," alifafanua. 

Bingwa huyo alisema uchunguzi hufanyika kabla ya IVF kwa jinsi zote. Huwa wanachunguza kwanza kubaini tatizo ndipo kuthibitisha haja ya upandikizaji. 

Alisema uchunguzi huo hujumuisha pia kuangalia wanawake ambao mji wa mimba huiharibu mbegu ya kiume ikiwa safarini kwenda kwenye yai kutunga mimba. 

Bingwa huyo pia alitaja wanaume kadhaa ambao mirija yao ina tatizo katika usafirishaji mbegu za kiume, hivyo hatua ya kuvuna mbegu hutumika. 

"IVF mara nyingi tunashauri wajifungue kwa upasuaji kwa sababu gharama kubwa imetumika, hatua ndefu, tunapunguza hatari ya mtoto huyo kupitia uzazi wa asili," alisema. 

Pia alisema upandikizaji hushauriwa uwe wa mtoto mmoja kutokana na kuchukuliwa tahadhari inayoweza kutokana na watoto pacha wawili au zaidi, kama vile kuzaliwa watoto njiti au ujauzito kuharibika. 

Akifafanua unavyofanyika upandikizaji huo, bingwa huyo alisema: "Kwanza, mayai kadhaa hupevushwa, labda mayai 10  na kuwa embrio, katika watoto 10 hatuwezi kukupandiza wote, tutahifadhi embrio (kiini tete).  

"Ikitokea utahitaji tena baada ya miaka miwili utakuja, au ikitokea dharura ujauzito umetoka tutakuwekea mimba nyingine.  

"Ila kuna gharama ya kuhifadhi embrio kwa ambao watahitaji huduma hiyo, labda wanakwenda kutafuta kwanza maisha, baadaye wanakuja kupandikiza." 

Kuhusu muda unaofaa kuanza mzunguko mpya wa IVF baada ya mzunguko wa awali ambao haukufanikiwa, bingwa huyo alisema ni baada ya mapumziko ya miezi miwili hadi mitatu. 

"Hakuna kikomo cha umri ingawa hali ya afya itatumika kufahamu kama mtu anaweza kupokea matibabu. Uwezekano wa kupata mimba hupungua kadri umri unavyosonga. Inachukua muda wa mwezi mmoja na nusu, ili kukamilisha mzunguko wa IVF. 

"Hii inajumuisha udhibiti wa homoni, sindano za kuchochea uzalishaji mayai na utaratibu kamili wa maabara ya IVF," alifafanua bingwa huyo.