TCB yaja na huduma za kidigitali maonesho ya 77

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 08:50 AM Jul 05 2024
Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya TCB, Francis Kaaya.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya TCB, Francis Kaaya.

BENKI ya Biashara Tanzania (TCB) imetangaza bidhaa mpya za kidigitali wanazotoa katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (sabasaba) zilizobuniwa ili kukidhi mahitaji ya wateja yanayoendelea kubadilika kila siku.

Bidhaa hizo ni ADABIMA ambayo ni mpango wa utoaji dhamana wa ada ambao TCB imeshirikiana na kampuni ya Metro Life Assurance ili kuwapa wazazi na walezi utulivu wa kiakili.

Nyingine ni KIKOBA bidhaa mpya, rahisi na yenye ufanisi ya kuweka akiba mtandaoni inayoboresha dhana ileile inayotumika katika vikundi vilivyozoeleka vya kuweka akiba na kukopeshana.

Mkuu wa Kitengo cha Bima Benki ya TCB, Francis Kaaya, ameyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akitangaza huduma mpya za kidigitali katika Maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayofanyika viwanja vya Mwalimu Nyerere.

Kaaya amesema benki hiyo, inajivunia kuwa moja ya washiriki wa Maonyesho ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendelea kwasababu yanatumika kutangaza fursa mbalimbali.

“Uwepo wa Rais Samia Suluhu Hassan na mgeni rasmi Rais wa Jamhuri ya Msumbiji, Filipe Nyusi, katika maonyesho ya mwaka huu, unadhihirisha dhamira thabiti ya serikali yake katika kukuza na kuimarisha chumi na kuboresha mazingira ya ustawi wa biashara ili kuchangia katika maendeleo ya nchi.

Benki ya TCB ni taasisi ya kifedha inayoongoza kwa kutoa bidhaa bunifu za kifedha zinazokidhi mahitaji ya wateja wake,” amesema.

Naye Mkuu wa Kitengo cha Uendeshaji wa Bidhaa za Kidigitali, Pray Henry Matiri, ameeleza kuwa, "Kikoba ni zaidi ya fursa ya kidigitali, kwani Kikoba inabeba dhana pana ya uwazi, jumuishi na usalama katika uwekaji wa akiba na simamizi bora wa kifedha.

“Tukitumia nyenzo hii ya teknolojia, tunaviwezesha vikundi nchini kote kusimamia mategemeo yao ya kiuchumi, kukua kiuchumi, na kujitegemea," amesisitiza