Waziri Mhagama awakumbusha wazazi kuendelea kusimamia malezi ya watoto

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:45 AM Jul 08 2024
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama Peramiho akifurahia jambo na Wanafunzi wa shule ya msingi Ligunga alipotembelea kujionea ujenzi wa miundo mbinu ya Maji, Madarasa na  Matundu ya vyoo.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama Peramiho akifurahia jambo na Wanafunzi wa shule ya msingi Ligunga alipotembelea kujionea ujenzi wa miundo mbinu ya Maji, Madarasa na Matundu ya vyoo.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Jenista Mhagama, Peramiho amehimiza Wazazi kuongeza ukaribu na usimamizi mzuri wa malezi kwa watoto ili kujua mienendo yao ya makuzi na kuwaepusha na makundi rika yenye ushawishi mbaya.

Waziri ametoa kauli hiyo wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini Mkoani Ruvuma ambapo amefanya mikutano Miwili ya hadhara katika kijiji cha Kizuka na Kitongoji cha Ligunga Jana Julai 07,2024.

“Vitendo vibaya vya uzalilishaji wa watoto vinafanyika mtaani, hivyo ni vyema tukawa tunafanya ukaguzi kwa watoto ili kujiridhisha usalama wao ikiwa ni pamoja na kufuatilia mabadiliko yao,” alisema Waziri Mhagama.

Amefafanua kwamba watoto ni baraka kutoka kwa Mungu, tuilinde baraka hiyo tuliyopewa na Mungu kwa kuzungumza nao kila wakati kuhusu makuzi yao.

Ukiona mtoto wako wa kiume na wakike ana mabadiliko ni vyema kufanya ufuatiliaji haraka kwa sababu tunabinadamu wenye mioyo na tabia za unyama na hawaoni dhambi kuharibu watoto wa wenzao.

Katika hatua nyingine Waziri Mhagama ameendelea kuhimiza vijana kuepukana na uraibu wa matumizi ya madawa ya kulevya ikiwemo bangi, ameeleza kwamba vitendo vyote visivyo na maadili hufanyika kutokana na ushawishi wa madawa ya kulevya.

“Wale wote ambao jamii inaona wameingia kwenye uraibu wa dawa za kulevya toweni taarifa ili waweze kupelekwa kwenye vituo vya utengamao vitakavyowasaidia kuachana na matumizi ya dawa za kulevya,”alisema Waziri Mhagama.

Kwa upande wake katibu Tawala wa Wilaya ya Songea Vijijini  Mtela Mwapamba ametoa rai kwa wananchi kuendelea kujitokeza kufuatilia vyeti vya kuzaliwa vya watoto ili viweze kuwasaidia pindi inapotokea uhitaji wa kutumia kwa shughuli mbalimbali.

“Sio mpaka mtoto amefaulu kwenda kidato cha kwanza, au anatakiwa kwenda Jeshi la Kujenga Taifa ndio mzazi unaanza utaratibu wa kutafuta cheti hiyo sio sawa lazima tuwe na vyeti vya vijana wetu mapema,” alisema Mwapamba