Diwani Kibaha apendekeza vituo elimu watu wazima kuanzishwa vijijini

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 04:18 PM Oct 05 2024
DIWANI wa Viti Maalumu Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Josephine Gunda
Picha: Julieth Mkireri
DIWANI wa Viti Maalumu Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Josephine Gunda

DIWANI wa Viti Maalumu Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Josephine Gunda amependekeza vituo vya elimu ya Watu wazima kuanzishwa ngazi ya Vijijini Ili wenye uhitaji wanufaike na fursa hiyo.

Gunda ametoa pendekezo hilo Jana Mjini Mlandizi wakati wa kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu ya watu wazima ambalo sherehe hizo zilijumisha utoaji wa vyeti kwa wahitimu 123.

Diwani huyo alisema sambamba na kuwepo kwa vituo hivyo pia Shirika la Kimataifa la DVV ambalo limeshiriki kufadhili maadhimisho hayo pamoja na  uwepo wa baadhi ya vituo vya elimu ya watu wazima wanatakiwa kufanyia shughuli hizo maeneo ya Vijijini Ili kuhamasisha wengine kujiunga kwenye vituo.

Alisema wapo watu wengi waliokosa fursa ya kusoma lakini kuwepo kwa vituo na ushuhuda kwenye maadhimisho kama hayo ni kichocheo kwao kubadilisha fikra zao na kuingia darasani.

Katika hatua nyingine Gunda aliishukuru Serikali kwa kuanzisha vituo hivyo ambavyo zaidi vinawasaidia watu waliokosa fursa kusoma na kujifunza masuala ya ujasiriamali yanayobadilisha maisha yao.

Atoa hamasa pia kwa Kampuni za gesi kuwa na uwakala maeneo ya Vijijini Ili kuwarahisishia wananchi kupata nishati hiyo kwa urahisi na kuondokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia 

Afisa Elimu Watu wazima Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha Meckitilda Kahindi alisema katika vituo 37 vilivyopo vya elimu ya Watu wazima  na kwa mwaka 2024 wameandikishwa wanakisomo 423.

Alisema katika Mpango wa wa uwiano kati ya elimu ya Watu wazima na Jamii wanaosoma kuanzia miaka 19 na programu nyingine za MEMKWA wengi wao wameweza kusoma na kuandika.

Kahindi pia alisema wamefanikiwa kuwa na shamba darasa ambalo wanajamii hujifunza mbinu Bora za kilimo na pia wamepata magonjwa vifaa vya TEHAMA kutoka kwa Shirika la kimataifa la DVV na kuwezesha Jamii kupata habari za kitaifa na kimataifa.

Afisa Miradi wa Shirika la DVV International Michael Mwalupale alisema wamekuwa wakisaidia uwepo wa vituo na utoaji wa Elimu ya watu wazima sambamba na kupata ujuzi wa ujasiriamali na Ufugaji wa samaki.

Aliwataka vijana ambao hawakupata fursa ya kusoma kutumia vituo vilivyopo ambavyo watapatiwa na ujuzi utakaowasaidia kuondokana na utegemezi.

Naye Subiraga Mwasongwe aliishukuru Serikali kwa kuanzisha vituo hivyo ambavyo vinatoa fursa kwa watu wote wakiwemo wenye Ulemavu .

Aliwasisitiza Wazazi kuondokana na dhana ya kuwatenga wenye Ulemavu na kuacha kuwapa haki yao ya Msingi ya elimu kwa madai kuwa hawawezi kusaidia kufanya kazi nyingine zaidi ya kukaa na kusubiri kuhudumiwa.