Bashe azindua Kituo Atamizi cha Mkonge Tanga

By Hamida Kamchalla , Nipashe
Published at 05:44 PM Oct 05 2024
Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe mara baada ya kuzindua Kituo  Atamizi cha Mkonge jana katika jengo la Bodi ya Mkonge jijini Tanga, wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Mkonge Sady Kambona, akifuatiwa na mkuu wa Wilaya ya Tanga Japhari Kubecha.
Picha: Hamida Kamchalla

SERIKALI imedhamiria kuwezesha zao la kimkakati la mkonge ambapo imetenga kiasi cha sh milioni 600 kwa ajili ya Kituo Atamizi cha Mkonge BBT - Tanga ili kukifanya kiwe kongano dogo la kuongeza thamani zao la mkonge pamoja na mazao mengine madogo madogo ya viungo.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amethibitisha hilo leo wakati akizindua kituo hicho kilichopo katika jengo la Bodi ya Mkonge jijini Tanga ambapo amesema serikali imeweka dhamira kukamilisha ombi la Bodi kwa pande zote mbili za Tanga na Zanzibar. 

"Kituo hiki kwa Mkoa huu patageuka kongano dogo ambalo litawekwa vifaa vyote vidogo vidogo vya kuongeza thamani mkonge na mazao mengine ya kilimo, hivyo fedha hii itakwenda kununulia vifaa na maligafi vitakavyo saidia wajasiria mali kutengeneza bidhaa zao, 

"Baada ya kuchukua mikopo yao,  wakina mama na vijana watakuwa wanakuja hapa na kila anayetaka kutengeneza bidhaa yake malighafi zote watazikuta hapa,  kwahiyo watatumia kama sehemu ya kuzalishia mali na kwenda kuuza kwenye biashara zenu" amesema.