Prof. Kabudi ataka ujenzi bweni Shule ya Msingi Sama kukamilika haraka

By Nebart Msokwa , Nipashe
Published at 04:01 PM Oct 05 2024

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi akipanda miti katika Shule hiyo.
Picha: Nebart Msokwa
WAZIRI wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi akipanda miti katika Shule hiyo.

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Kyela mkoani Mbeya kukamilisha haraka ujenzi wa Bweni la wanafunzi wa kike wenye mahitaji maalumu wa Shule ya Msingi Sama ili kuwapunguzia kero ya kusafiri umbali mrefu kwenda shuleni.

Prof. Kabudi ametoa agizo hilo alipoweka jiwe la msingi la ujenzi wa bweni hilo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi, kuzindua na kuweka mawe ya msingi kwenye ujenzi wa miradi mbalimbali mkoani Mbeya.

Jengo hilo linajengwa kwa gharama ya zaidi ya Sh. Milioni 100 ambapo alisema jengo hilo linatakiwa likamilike kabla ya mwezi januari ili wanafunzi hao waendelee kulitumia.

Amesema lengo la serikali ni kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu kwa wanafunzi wote bila kujali hali zao huku akisisitiza kuwa elimu ni haki ya kila mtoto kwa mujibu wa sheria za nchi.

“Nimeambiwa bado Sh. Milioni 30 kwa ajili ya kukamilisha jengo hili, mkurugenzi hakikisha unaleta fedha hizo haraka ili jengo likamilike, mwezi januari jengo lianze kutumika, hakuna kisingizio hapa,” amesema Prof. Kabudi.

Amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya uboreshaji wa sekta ya elimu na hivyo akawataka viongozi wa serikali kuhakikisha wanasimamia fedha hizo ili zilete matokeo Chanya.