Fadlu: Hatuna wa kumlaumu

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 09:11 AM Oct 06 2024
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.
Picha:Simba
Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids.

BAADA ya sare ya kushangaza dhidi ya Coastal Union, Kocha Mkuu wa Simba, Fadlu Davids, amesema hawana wa kumlaumu katika mchezo huo, huku akisema ana kazi ya kufanya ili kubadili mitazamo ya wachezaji wake.

Akizungumza baada ya kumalizika kwa mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara kati ya timu hiyo dhidi ya Coastal Union, ikiisha kwa mabao 2-2, Fadlu, alisema wachezaji wake walicheza kwa kuridhika na kuichukulia poa mechi hiyo.

Alisema wachezaji wake walitakiwa waimalize mechi hiyo kipindi cha kwanza kwani walikuwa na uwezo wa kufunga zaidi ya mabao mawili, lakini hawakufanya hivyo, badala yake wakaonekana kama wameimaliza mechi kabla ya mabao mawili ya kushtukiza yaliyoonekana kuwachanganya.

“Mechi ilitakiwa kumalizwa kipindi cha kwanza kwa kufunga goli la tatu, lakini kwa kilichotokea nina kazi ya kubadili mitazamo ya wachezaji, tutarudi uwanja wa mazoezi kujiandaa kuelekea mchezo ujao dhidi ya Yanga," alisema kocha huyo.

Hata hivyo alisema ana kazi kubwa kuelekea mchezo huo wa Oktoba 19, kwani wachezaji wengi wanakwenda kwenye vikosi vya timu za taifa, hivyo atabaki na baadhi ya wachezaji tu.

"Hakuna la kufanya, tutaendelea na mazoezi na hawa waliopo kuelekea kwenye mchezo huo muhimu," alisema Fadlu.

Kwa upande wa Kaimu Kocha Mkuu wa Coastal Union, Joseph Lazaro, alisema Simba waliingia kwenye mtego, ndiyo maana walifanikiwa kurudisha mabao yote mawili na ingewezekana wangeweza kupata hata la tatu.

"Kikubwa ni kwamba tuliwaheshimu hasa kipindi cha kwanza, sasa wakaingia kwenye mtego kudhani tutakuja hivyo hivyo kipindi cha pili. Matokeo yake tulibadilika na kushambulia, mabao yote ni ya kushtukiza, wao walijua sisi tutakuwa tunakaba tu muda wote kama ilivyokuwa kipindi cha kwanza," alisema kocha huyo ambaye alikuwa beki wa kushoto wa zamani wa timu hiyo.

 Mabao ya kipindi cha pili ya Hassan Abdallah na Ernest Malonga, yaliiwezesha Coastal Union kurudisha mabao yote mawili waliyofungwa kipindi cha kwanza na Mohamed Hussein 'Tshabalala', na Leonel Ateba na kuifanya mechi hiyo iliyochezwa juzi, Uwanja wa KMC Complex, Mwenge, Dar es Salaam kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 na kuwashangaza wanachama na mashabiki wa Simba waliokuwa uwanja ni hapo na waliokuwa wakiangalia kwenye televisheni.

Sare hiyo inaifanya Simba kupanda hadi nafasi ya pili ikifikisha pointi 13 kama Fountain Gate na kuishusha kwenye nafasi hiyo kutokana na kuwa na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.

Pamoja na sare hiyo, bado Coastal Union inasalia nafasi ya 13 ikifikisha pointi tano, ikiwa ni sare ya pili kwenye Ligi Kuu.