Majaliwa aagiza lori likaondoe madawati shuleni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:59 PM Jul 08 2024
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, (wa tatu kushoto) akikagua madawati katika shule ya sekondari ya Iramba Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, (wa tatu kushoto) akikagua madawati katika shule ya sekondari ya Iramba Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameagiza kuondolewa kwa madawati yaliyopo katika shule ya sekondari ya Iramba Wilaya ya Mufindi Mkoani Iringa ambayo hayana eneo la kuhifadhi madaftari ya wanafunzi.

Agizo hilo amelitoa jana mkoani Iringa wakati akizindua shule ya wasichana ya Iramba baada ya kubaini kuna madawati ambayo hayana eneo la kuhifadhia madaftari ya wanafunzi.

“Nimeingia darasani nimekuta madawati mmeniambia dawati moja Sh 50,000. Madawati ya shule za msingi na sekondari ni lazima yawe na maeneo ya kuweka madaftari ya wanafunzi akikaa juu kuwe na daftari la kuandika ama kitabu,”amesema Majaliwa.

Amesema amejulishwa kila dawati ni Sh 50,000 mengine yanayo sehemu ya kuhifadhia na mengine hayana na gharama zilizotumika ni hizo hizo haiwezekani kukubalika.

Kassim.jpeg 336.37 KB
“Nikitoka hapa leteni lori muondoe haya madawati yote yasiyokuwa na maeneo ya kuhifadhia madafri yao myarudishe kwa fundi. Nimesema yarudishwe kwa fundi Mwenyekiti wa Halmashauri simamia hili fedha mmetoa ninyi na usimamizi lazima msimamie,”.

Majaliwa alimtaka ofisa elimu kuhakikisha anasimamia jambo hilo, anavyoondoka madawati hayo yaondolewe na kuletwa lenye eneo la kuhifadhi madaftari ya wanafunzi hao.

“Hili ni jambo kubwa ambalo sikuridhika nalo leo ofisa elimu lichukue hilo ni suala lako,”amesema Majaliwa.