SHIRIKA lisilo la kiserikali la AMREF Health Africa-Tanzania, limetia saini hati ya makubaliano na East Africa Television Limited (EATV) yakilenga kutengeneza maudhui yanayohusu elimu ya afya, maji na usafi wa mazingira hasa kwa vijana na wanawake nchini.
AMREF Tanzania ambao ni wadau wakubwa wa maendeleo wanaoshirikiana na serikali, wamefurahishwa na kazi kubwa inayofanywa na East Africa TV, East Africa Radio na mitandao yake ya kijamii katika kuyafikia makundi mbalimbali ya watu hasa kundi kubwa la vijana.
Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, Tanzania iliripotiwa kuwa na vijana asilimia 77.
Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika kati ya Mkurugenzi Mkazi wa AMREF Tanzania, Dk. Florence Temu na Mkurugenzi Mtendaji wa East Africa Television Ltd, Regina Mengi, katika ofisi za EATV, Mikocheni jijini Dar es Salaam.
Dk. Florence na ujumbe wake pia walitembelea vituo vya East Africa TV na East Africa Radio na kujionea uwekezaji mkubwa uliofanywa pamoja na uzalishaji wa vipindi vinavyoruka kila siku hewani.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Florence alisema wamejifunza mambo mengi katika ziara hiyo kwa kujionea vipindi mbalimbali vinavyotayarishwa.
“Ndio maana nilisema pale usione vinaelea vimeundwa, unaweza kusema mbona gharama za media kubwa, lakini nimeona uwekezaji mliofanya si tu wa vifaa, hata aina ya watumishi mnaowahitaji ni wenye elimu zao na ujuzi.
“Nimefurahi wote ni Watanzania wanafanya kazi za viwango vya hali ya juu na mmetoa ajira kwa vijana, inahamasisha hasa mlivyoeleza mlikoanzia na mmeendelea kukua na kuikamata teknolojia, hii imetupa hamasa,” alisema.
Dk. Florence alisema AMREF ni shirika lisilo la kiserikali na si la faida, lakini kinachofanyika kinaleta matokeo chanya ndani ya jamii.
“Tunashirikiana na serikali kwa karibu ikiwamo Wizara ya Afya, Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na nyingine zinazohusika na jamii zikiwamo zinazojihusisha na mazingira, utendaji kazi wetu lengo kubwa ni kumfikia mwanajamii, na ngazi tunayopitia ni kinamama na vijana, hapo tunaunganisha mabinti na watoto,” alifafanua.
Dk. Florence alisema wanapotembelea studio hizo na kukuta vipindi vya kinadada, kinamama na vijana, huku jamii nzima ikiangalia inaleta hamasa kubwa.
“Tunashukuru namna mnavyotupa ushirikiano, tukiwa na matukio ndani ya AMREF tunashirikiana na vyombo vyenu, na ninyi mnatushirikisha kwenye programu zenu mfano kampeni yenu ya Namthamini,” alisema.
Alisema kupitia ushirikiano walioingia utaunganisha nguvu, ikiwamo katika kutafuta rasilimali fedha, rasilimali watu na teknolojia.
“Ndio maana tunasema nguvu ya media ni kubwa, tunapotengeneza makala zinaweza kwenda mbali zaidi na tuna miradi yenye matokeo chanya mfano afya ya mama na mtoto, masuala ya mazingira safi, magonjwa ya maambukizi ikiwamo HIV na TB (Kifua Kikuu). Tunapokuwa na makala kama hizo watu wakiangalia wanapata mahali pa kujifunza,” alisema.
Dk. Florence alisema vyombo vya habari ni muhimu katika afua za kiafya na katika kufikisha taarifa za mabadiliko ya tabia ya jamii ili kuwa na afya bora.
Mkurugenzi Mtendaji wa East Africa Television Limited, Regina alipongeza shirika hilo kwa kuchangua kufanya kazi na East Africa Television Ltd, kwa kuwa vyombo vyake vinawafikia watu wengi katika kuhabarisha na kuelimisha.
Aidha, alimhakikishia Mkurugenzi wa AMREF kuwa wapo tayari kuendelea kufanya kazi nao kufikisha ujumbe ambao umekusudiwa katika kuleta mabadiliko ya maisha ya kinamama na vijana.
Alisema wanaamini kwa ushirikiano wao watafikisha ujumbe mzuri zaidi kwa jamii kupitia makala na vipindi vinavyoruka katika kituo hicho.
“Bahati mbaya sana afya tunaiangalia baada ya kupata tatizo badala ya kuelimika na kujilinda na matatizo yanayoweza kutokea. Afya ya akili nayo tunaona imekuwa ni changamoto kubwa.
“EATV tunategemea tutajifunza mengi kutoka kwenu ya namna ya kuwakilisha na kufikisha ujumbe kwa jamii, tukiwa na nia ya kukuza na kulea jamii kwa ujumla ili iwe na afya bora na kuchangia katika ustawi wa jamii kwa ujumla,” alisema Regina.
East Africa Television Ltd imeendelea kufungua milango ya ushirikiano na taasisi za kiserikali, zisizo za kiserikali, kampuni na wadau binafsi katika kutumia vyombo vyake vya East Africa Television, East Africa Radio na mitandao yake ya kijamii ili kuwafikia watu wengi zaidi hapa nchini katika kuwaelimisha na kuwahabarisha.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED