WMA yanunua mitambo ya kisasa kupimia mita za umeme

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:59 AM Jul 05 2024
Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA), Kitengo cha Bandari,  Alfredy Shungu (wakwanza kulia) akitoa elimu ya vipimo jana kwa mdau alipotembelea banda la WMA katika maonesho ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam. katikati ni Meneja Sehemu ya Upimaji.
Picha: Mpigapicha Wetu
Meneja wa Wakala wa Vipimo (WMA), Kitengo cha Bandari, Alfredy Shungu (wakwanza kulia) akitoa elimu ya vipimo jana kwa mdau alipotembelea banda la WMA katika maonesho ya sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam. katikati ni Meneja Sehemu ya Upimaji.

KATIKA jitihada za kwenda na mabadiliko ya teknolojia duniani kwenye masuala ya vipimo Wakala wa Vipimo (WMA), imenunua mitambo mitatu ya kisasa ya uhakiki wa mita za umeme.

Hayo yamesemwa leo kwenye Maonyesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa na Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa (WMA), Paulus Oluochi, wakati akizungumza kwenye maonyesho hayo.

Oluochi alisema mitambo miwili ipo katika Kituo cha uhakiki eneo la Misugusugu Mkoa wa Pwani na mtambo mmoja upo Mkoani Kilimanjaro.

Alisema kununuliwa kwa mitambo hiyo kumeleta ufanisi mkubwa kwenye eneo la uhakiki wa mita za umeme na kwamba tayari wameshaanza kuhakiki mita hizo tangu mwezi wa tatu mwaka huu.

Alisema kuanzia mwezi wa tatu mwaka huu mita zote zinazotoka nje ya nchi na zile zinazotengenezwa nchini zimekuwa zikihakikiwa na WMA ili kuhakikisha hazimpunji mteja wa mwisho.

“Uhakiki wa mita mpya za umeme lilianza mwezi Machi na zaidi ya mita 2,000 zimeshahakikiwa ikiwa ni utekelezaji wa Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 na mita zote kabla ya kufungwa kwa wateja zinakuja kwetu tunazipima na kama hazina shida zinafungwa kwa wateja,” alisema Oluochi.

Wakala imeendelea kutoa elimu ya usahihi wa vipimo na kuwataka wafanyabiashara waache tabia ya lumbesa

Oluochi alisema WMA imekuwa ikifanya operesheni za mara kwa mara kukagua kama wafanyabiashara wanazingatia vipimo sahihi na wale wanaokutwa wakikiuka hutozwa faini.

Alisema kwenye  maonesho hayo, Wakala wa Vipimo inajikita katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya vipimo katika maeneo mbalimbali ya biashara, afya, mazingira na usalama, kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala mbalimbali ya vipimo.

Alisema lengo la WMA ni kuwajengea ufahamu wadau na wananchi kwa ujumla juu utendaji kazi wa WMA katika uhakiki wa Mita za Umeme, Dira za Maji na vipimo vingine mbalimbali.

Shungu alisema katika namna ya kipekee, WMA pia inaendelea kutoa elimu  kwa wadau na wananchi kwa ujumla juu ya ufungashaji sahihi wa mazao katika uzito wa kilogramu 100 kama Sheria ya Vipimo Sura Na. 340 inavyoelekeza na wajiepushe kufungasha mazao ya shamba kwa uzito unaozidi kiligramu 100 maarufu kama Lumbesa kwani kufungasha hivyo ni kosa kisheria.

Kadhalika, alisema WMA inaendelea kutoa elimu kwa wauzaji wa mazao mbalimbali kuuza kwa kutumia mizani sahihi iliyohakikiwa na siyo kwa kutumia makopo, visado na ndoo na wito unatolewa kwa wanunuzi wote wa bidhaa  kutumia mizani katika manunuzi yao yote katika masoko na maduka ya kuuzia bidhaa.

“WMA inawakaribisha wadau wa vipimo na wananchi wote kutembelea banda lakelililopo ndani ya banda la Wizara ya Viwanda na Biashara katika viwanja vya SabaSaba ili kuweza kujipatia elimu na ushauri wa kitaalamu juu ya masuala mbalimbali ya vipimo,” alisema.

Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba) yamefunguliwa Rasmi Julai 3, 2024  na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi ambaye aliambatana na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.