Makonda: Kuna watu biashara ya kuku iliwashinda kazi yao kuwaumiza wawekezaji

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 06:59 AM Jul 05 2024
Mkuu wa Mkoa Arusha, Paul Makonda.

Mkuu wa Mkoa Arusha, Paul Makonda, ameagiza wawekezaji wasichukuliwe kama maadui wanapokuwa wanafanya biashara zao.

Makonda ameyasema hayo wakati wa uzinduzi wa ofisi ya kituo cha uwekezaji (TIC) na awamu ya pili ya kampeni ya uhamasishaji uwekezaji wa ndani jiji Arusha.

“Awe mwekezaji wa ndani ama nje ya nchi tusiwafanye kama maadui, tusiwaumize wawekezaji wetu kuna kipindi huwa nawaza itafika wakati tutaomba muongozo serikalini kabla ya mtu kuteuliwa tumuulize ulishawahi kufanya biashara gani iwe ni moja ya sifa,”amesema Makonda na kuongeza kuwa;

“Kwa sababu kuna watu hata biashara ya kuku hawajawahi kuiweza lakini akiingia kwenye biashara ya mtu anamsumbua utazani amekutana na shetani anamshughulikia ili ampeleke motoni. Kuna watu wanapata shida wakati wameajiri watu hata mtu akitaka kupatiwa utaratibu imekuwa ni shida,".

Alisema unakuta mtu anatafuta zake mtaji ama kuuza kiwanja chake na kuanza biashara, hivyo wanapokuja watu wa serikali wawasaidie na sio kutafuta njia ya kuwarudusha nyuma.

“Niombe kwenye hiki kituo cha uwekezaji ambacho mimi nina imani nacho kwa asilimia 100 watendaji wengine wa taasisi wanatakiwa kujua unalipwa mshahara kwa kodi za wafanyabiashara tuwahudumie vizuri na sio kuwaumiza,”alisema Makonda.

Makonda alisema anachokitamani ni kuona kituo hicho kinakuwa cha kwanza kwa ubora kwa Afrika kwa kutengeneza watalii wengi zaidi na kiwe na watumishi wenye weledi hawataki kuwa na watu wanaorudisha nyuma maendeleo ya uwekezaji.