Hadhari yatolewa wazazi wa watoto njiti na pacha

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 07:11 AM Jul 05 2024
Mtoto Njiti.
Picha: Mtandao
Mtoto Njiti.

BINGWA wa Magonjwa ya Macho Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk. Neema Moshi, ametoa angalizo kwa jamii, hasa kinamama wanaojifungua watoto chini ya wiki 34 (njiti) na pacha wawili au zaidi, kujihadhari na hatari ya watoto hao kukumbwa na upofu.

Bingwa huyo anasema watoto njiti, pacha zaidi ya wawili wanaozaliwa kabla ya miezi tisa kama ilivyo kibaiolojia, pazia lao la nyuma la kuonea (retina), huwa halijakamilika kuundwa, hivyo kuhitaji kuanza tiba siku 28 baada ya kuzaliwa.

Akizungumza na Nipashe katika Banda la MNH kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar es Salaam (DITF) jana, Dk. Neema alisisitiza kinamama kuhakikisha watoto waliozaliwa kabla ya wakati na pacha kufanya uchunguzi wa macho kuwaepusha na upofu.

Bingwa huyo alisema kuwa msimu huu wa Sabasaba, elimu wanayotoa kwa umma inagusa tatizo hilo, pia kukumbusha wasaidizi wa afya, wakunga kwamba kinamama wanaojifungua aina hiyo ya watoto, wafike kwa mtaalamu wa macho kufanyiwa uchunguzi. 

"Upo upofu kwa watoto unaosababishwa na kuzaliwa kabla ya wakati au umri wa mimba kutimia au njiti wanaozaliwa chini ya wiki ya 34, mara nyingi pazia lao la kuonea, kitaalamu retina, huwa halijakomaa. 

"Kwahiyo, inategemea kuna ambao pazia litakomaa bila kupata athari zozote, na wapo ambao litakomaa lakini kwa shida, asipotibiwa haraka, anaweza kupata upofu kwa maisha yake yote.

"Hivi sasa watoto wenye shida hizi kwanini tunawabaini kipindi hiki? Ni kwa sababu zamani watoto njiti waliozaliwa walikuwa ni nadra kupona kutokana na vifaa duni. Wengi wanaozaliwa hivi sasa wanapona na wanafikia umri mkubwa, vifaa vipo," alisema. 

Bingwa huyo alieleza zaidi kuwa watoto hao hata kama wameruhusiwa kutoka hospitalini, wataendelea kuchunguzwa hadi wanapovuka wiki ambazo zilitakiwa wazaliwe, ili kuimarisha uwezo wa pazia la kuona. 

Alitaja makundi ya walio hatarini kukumbwa na shida hiyo ni kwa waliozaliwa chini ya uzito mdogo zaidi usiovuka kilo mbili, mimba chini ya wiki 34 ambao huhitaji kuchunguzwa hadi pazia linapokomaa. 

Bingwa huyo alisema kuwa katika kliniki ya macho Muhimbili, huwaona takribani watoto 10. 

Dk. Neema alisema wengine walio katika hatari ya upofu ni watoto walio na shida ya upumuaji na wanaoongezewa damu kama vile pacha zaidi ya wawili, ambao mara nyingi huwa njiti; wana hatari ya kupata upofu wasipotibiwa.

"Tunashauri wakati daktari wa watoto anaendelea kuwachunguza, basi pia mtaalamu wa macho tushirikiane kuchunguza watoto hawa iwapo pazia lao liko sawa. Tiba ya tatizo hili ni pamoja na mionzi ya jicho na sindano. 

"Akiendelea na tiba, ukuta utarejea na iwapo matibabu hayatafanyika katika wiki chini ya 34 anaweza akahitaji matibabu makubwa zaidi ya upasuaji kurudishia pazia ambalo huwa limejificha.  

"Iwapo tiba itachelewa zaidi, hata hilo pazia linakuwa limeshaondoka hulipata tena, atakuwa na upofu maishani. 

"Kama mtoto aliumwa sana akiwa njiti, baada ya siku 28 za kuzaliwa aonwe na mtaalamu wa macho. Hata kama mtoto yuko hospitalini na anapata msaada wa mashine ya oksijeni, lazima achunguzwe hili, ili kuwahi pazia lake kabla halijaondoka, pazia hujitengeneza kiasili kwa muda maalum," alisema Dk. Neema. 

Bingwa huyo alisema kuwa hatua za ukuaji wa mtoto kutoka wiki ya kwanza hadi miezi tisa, ndiyo nguzo imara ya kila kiungo kinachounda mwili wake kwa kipindi maalum, hivyo wanaozaliwa chini ya wiki 34 ni rahisi kuwa na hitilafu kama vile retina kutokamilika kujitengeneza.