Jamhuri yapewa nafasi ya mwisho kesi ya Malisa, Meya Jacob ifutwe

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 07:07 AM Jul 05 2024
Mfanyabiashara na mwanasiasa Boniface Jacob na mwenzake, mwanaharakati Godlisten Malisa wakiwa nje ya Mahakama.
Picha: Mpigapicha Wetu
Mfanyabiashara na mwanasiasa Boniface Jacob na mwenzake, mwanaharakati Godlisten Malisa wakiwa nje ya Mahakama.

MEYA wa zamani wa Manispaa ya Ubungo, Dar es Salaam, Boniface Jacob na Godlisten Malisa wamelalamika Upande wa Jamhuri kushindwa kuwasomea maelezo ya awali mara tatu mfululizo katika kesi inayowakabili ya kusambaza taarifa za uongo mtandaoni kwa lengo la kupotosha umma.

Washtakiwa hao wamedai kitendo hicho ni kuwasumbua kwa sababu sheria iko wazi kwamba upande wa mashtaka na polisi unatakiwa wafanye nini kabla kesi haijafikishwa mahakamani.

Malalamiko hayo waliyatoa jana mbele ya 

Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swalo wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kupita Wakili wao, Peter Kibatala wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo hayo.

Wakili wa Serikali Frank Michael alidai kuwa hawawezi kuendelea na PH (usikilizwaji wa awali) dhidi ya washtakiwa kwa kuwa jalada limeitishwa kwa ajili ya mapitio, hivyo wakaomba iahirishwe na wapangiwe tarehe nyingine.

"Hiyo PH inaahirishwa mara tatu mfululizo, sheria iko wazi kwa upande wa mashtaka na polisi kama watakuwa hawajakamilisha upelelezi, basi wasiwapeleke watuhumiwa mahakamani isipokuwa makosa makubwa, kwa sababu mapitio yalitakiwa yafanywe kabla ya kesi kuletwa mahakamani," alidai Kibatala. 

Wakili huyo alidai kuwa kitendo hicho ni kusumbua washtakiwa, wanakwenda mahakamani lakini hakuna kinachoendelea. Akaoma mahakama itoe amri kwamba, kama itaridhia ahirisho hilo la Jamhuri, basi liwe la mwisho.

"Na kama siku itakayopangwa kesi haitoendelea basi nitatoa hoja kwamba washtakiwa waachiwe chini ya Kifungu Na. 226 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA)," alidai Kibatala.

Baada ya kusikiliza hoja za kila upande, Hakimu Swalo alitoa maelekezo kuwa anatoa ahirisho la mwisho na pia ni kweli PH imeahirishwa mara tatu. Akaahirisha kesi hiyo hadi Julai 30 mwaka huu na kama upande wa Jamhuri hautaendelea siku hiyo, atafuata sheria kama inavyoelekeza.

Katika kesi hiyo, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka matatu, likiwamo la kusambaza taarifa za uongo mtandaoni kwa lengo la kupotosha umma kuhusiana na kijana aliyedaiwa kupotea.

Ilidaiwa kuwa Aprili 22 mwaka huu, ndani ya Mkoa na Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa Jacob, kwa lengo la kupotosha umma, alisambaza taarifa ya uongo kupitia mfumo wa kompyuta wenye jina la Boniface Jacob @ExmayorUbungo wenye kichwa kilichosomeka 'wenye leseni ya kuua wameua tena'.