Tume ya Mipango yahakikishia usiri watoa maoni Dira ya 2050

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:22 AM Jul 05 2024
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba akiteta jambo na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Laurence Mafuru.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba akiteta jambo na Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Laurence Mafuru.

TUME ya Mipango imewahakikishia wananchi usiri katika maoni watakayoyatoa kwa ajili ya kutengeneza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Laurence Mafuru, alisema hayo jana wakati wa kikao cha Kamati ya Usimamizi wa Dira, kwenye kikao cha Wajumbe wa Tume ya Mipango, Timu ya Kuu ya Kitaalamu na Uandishi wa Dira ya Maendeleo 2050.

Aidha, amewataka wananchi kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao katika mfumo tofauti uliowekwa, ili kuhakikisha kila mmoja anashiriki kutengeneza nyaraka hiyo muhimu kwa maendeleo ya taifa.

Wajumbe hao walikutana kwa ajili ya kupata picha kamili ya walipotoka na wanapokwenda katika kutengeneza dira hiyo, katika mkutano ulioongozwa na Prof. Mkumbo na kuhudhuriwa na wajumbe wake akiwamo Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba aliyehudhuria kama mjumbe.

“Na sisi kama tume pekee bila wizara hatuwezi kusonga mbele. Tumekutana ili kujadili kwa kina na kujiwekea mkakati na malengo ambayo si yakufikirika, lakini kutekelezeka,” alisema.

Alisema wananchi wanaombwa kujitokeza kwa wingi kutoa maoni yao kwa kuzingatia vipengele vya dodoso, huku wakitakiwa kuongeza maelezo na taarifa za ziada ambazo ni muhimu kuzingatiwa katika Dira hiyo.

“Taarifa watakazotoa wananchi zitatumika katika maandalizi ya Dira na hivyo nawahakikishia usiri wa taarifa zao. Serikali inatambua kuwa, maono na maratajio ya Watanzania na mbinu za kuyafikia zinatokana na Watanzania wenyewe kupitia ushirikishwaji madhubuti katika maandalizi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mafuru, ili kuhakikisha Dira hiyo inabeba maono na matarajio ya Watanzania kwa miaka 25 ijayo, ni muhimu wananchi na wadau wote wa maendeleo kushirikishwa kikamilifu katika mchakato wa maandalizi ya Dira tangu hatua za awali hadi kukamilika kwake.

“Lengo la kikao hiki ni kuangalia mambo muhimu ambayo matarajio yetu kama nchi yaliweka na kuangalia kama yalifikiwa na kuangalia sasa kule tunakokwenda na yale tunayoyachukua kuendelea nayo mbele,” alisema.

Alisema kinachotakiwa ni kuangalia maoni na kuwa na sura halisi ya uchumi sanjari na malengo yanayotarajiwa kuyaona.