Mhitimu VETA abuni mashine kutunzia watoto njiti

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 02:56 PM Jul 02 2024
Mhitimu wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA Mkoa wa Arusha, George Nyahende, akionyesha mashine aliyobuni mwenyewe ya kutunza watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao yaani njiti wakati wa maonyesho ya biashara ya kimataifa yanayoendelea.
PICHA: JOSEPH MWENDAPOLE
Mhitimu wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA Mkoa wa Arusha, George Nyahende, akionyesha mashine aliyobuni mwenyewe ya kutunza watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao yaani njiti wakati wa maonyesho ya biashara ya kimataifa yanayoendelea.

MHITIMU wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA Mkoa wa Arusha, George Nyahende, amebuni mashine ya kutunza watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao yaani njiti.

Akizungumza na Nipashe Digital hili leo kwenye maonyesho ya kimataifa yanayondelea kwenye Viwanja vya Mwalimu JK Nyerere jijini Dar es Salaam, Nyahende,  amesema kwenye mashine hiyo , ameweka teknolojia mpya ambayo mashine zinazotoka nje ya nchi hazina. 

Amesema baada ya kuhitimu VETA aliajiriwa kwenye kampuni moja mkoani Arusha lakini baada ya muda aliamua kuacha kazi mwenyewe na kujiajiri kwa kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali.

 Amesema amekuwa na kawaida ya kudadisi matatizo mbalimbali yaliyoko kwenye jamii na kuyatafutia ufumbuzi na kuongeza kuwa hali hiyo imemwezesha kuvumbua vitu mbalimbali ambavyo vimeleta suluhisho kwenye jamii.

Amesema alipata wazo la kutengeneza mashine ya kutunzia watoto hao baada ya daktari wa Hospitali ya Mount Meru Arusha kumweleza kuwa hospitali hiyo haina mashine ya aina hiyo kwani inauzwa bei kubwa.

“Hapo wazo likaja nitengeneze mashine hiyo nikaitengeneza nikaenda Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) wakaniambia nianzishe kiwanda kidogo nikaanzisha na sasa hivi nimefikia hatua nzuri ambayo watanipa usajili ili niweze kutengeneza mashine nyingi na kuuza kibiashara,” amesema

Amesema TMDA walimtaka kulinganisha matumizi ya mashine yake na zile zinazotumika kwenye hospitali mbalimbali ili kuangalia kama zinafanyakazi sawasawa na kwamba baada ya kufanya hivyo aliwaandikia ripoti inayoonyesha kuwa zinaweza kutumika hospitali.

“Nimetengeneza moja tu kama mfano ila kibali kitakapotoka ndipo nitaanza sasa kuzalisha nyingi kwaajili ya biashara, kwa kawaida moja inafikia hadi milioni 80 lakini watakaonunua kwangu sitawauzia zaidi ya shilingi milioni 10,” amesema na kuongeza.

“Nimeijaribu mashine hii kwenye hospitali ya Arusha Medical Center na St. Elizabeth na madaktari na wataalamu wa hospitali hizo walipolinganisha walithibitisha kwamba inafanyakazi sawa sawa waliandika ripoti na nikaiwasilisha TMDA,” amesema

Amesema kwenye kutengeneza mashine hiyo alitumia malighafi zinazopatikana hapa hapa nchini ili atakapoanza kutengeneza kwa wingi asitumie gharama kubwa ili aziuze kwa gharama ndogo kuwezesha kampuni na hospitali nyingi wamudu kuzinunua.

Amesema ameongezea thamani mashine hiyo  kwa kuweka vitu mbalimbali hali ambayo imeipa ubora wa hali ya juu kulinganisha na mashine zinazotoka nje ya nchi ambazo alisema ziko kibaishara zaidi.

“Kwa mfano kwenye zile za nje mtoto anapokuwa kwenye hii mashine wakitaka kumpita uzito wanamtoa nje ya mashine wanaenda kumpima sehemu zingine na kumrudisha ndani ya mashine lakini hii ya kwangu nimeweka mzani ambao uzito wa mtoto unaonekana akiwa humo humo hakuna haja ya kumtoa nje,” amesema 

“Kingine ni kama mtoto aliyeko kwenye mashine hii anashida ya kupumua wao wanamwekea mipira mimi nikaona haina haja kwa hiyo nikabuni namna ya kumpa hewa akiwa humohumo bila kumweka mipira anapata hewa akiwa amelala na teknolojia hii mashine za nje hawajaweka,” amesema

Amesema kabla ya mlipuko wa COVID akiwa mkoani Arusha mwanamke mmoja aligongwa na nyoka lakini alipopelekwa hospitali alifariki na alipodadisi madaktari walimwambia kuwa amekufa kwasababu hawakuwa na mashine ya kumsaidia kupumua.

“Niliwauliza huku hakuna umeme hata zikiletwa hizo mashine mtazitumiaje wakasema ndiyo maana hazijaletwa basi kuanzia hapo nikapata wazo la kutengeneza mashine ya kumsaidia mgonjwa kupumua ambayo inaweza kufanyakazi kwa kutumia betrii na isiyohitaji mitungi ya oxygen,” amesema