Kituo cha uwezeshaji wanawake kiuchumi kupitia uzalishaji sabuni chazinduliwa

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 11:53 AM Jul 04 2024
Afisa tarafa wa Shinyanga Mjini Telezia Alois akikata utepe kuzindua Kituo cha Uwezeshaji Wanawake kiuchumi kupitia uzalishaji Sabuni za Maji
Picha: Marco Maduhu
Afisa tarafa wa Shinyanga Mjini Telezia Alois akikata utepe kuzindua Kituo cha Uwezeshaji Wanawake kiuchumi kupitia uzalishaji Sabuni za Maji

SHIRIKA la Tanzanian Youth and Children (TYC) limezindua Kituo cha Uwezeshaji Wanawake kiuchumi kupitia uzalishaji wa sabuni za maji “Jamii Soap”

Uzinduzi huo umefanyika jana na kuhudhuliwa na wanawake Wajasiriamali, wakiwamo wale ambao awali walishapewa mafunzo ya uzalishaji sabuni na shirika hilo.

Mkurugenzi wa Shirika la TYC, Lucas Daudi, alisema wapo kweye utekeleza wa mradi wa kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia  uzalishaji wa sabuni, kwa ufadhili wa Tanzania Development Trust, ndiyo maana wanawajengea wanawake ujuzi wa kuzalisha sabuni za maji ili wapate kipato na kuondokana umaskini.

Amesema kabla ya kutekeleza Mradi huo walifanya utafiti na kugundua kwamba asilimia 87 ya sabuni hapa nchini zinatoka Nje ya Nchi, lakini Malighafi za utengenezaji wa Sabuni hizo  zinatoka hapa hapa Tanzania.

“Baada ya kufanya utafiti na kugundua Tanzania kuna uhitaji mkubwa wa sabuni, ndipo tukaja na mradi wa kuwajengea wanawake ujuzi wa uzalishaji sabuni ili watumie fursa hiyo kujikwamua kiuchumi.” alisema Daudi na kuongeza kuwa;

“Mradi huu umejikitika kabisa kwa Wanawake sababu ndiyo waathirika wakubwa wa uchumi na wana mahitaji mengi, hivyo wakijikwamua kiuchumi hata vitendo vya ukatili vitapungua, sababu chimbuko la ukatili ni umaskini,”aliongeza.

Mjumbe wa Bodi wa TYC Ntimba Daniel, alisema kupitia Kituo hicho pia wanawake watajengewa uwezo wa kuendesha Biashara zao pamoja na mbinu za kupata Masoko, na kitatoa fursa ya Ajira kwa vijana.

Mgeni rasmi Afisa Tarafa wa Shinyanga Mjini ,Telezia Alois akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, alilipongeza Shirika hilo kwa kumkomboa mwanamke kiuchumi,na kwamba mwanamke akiwezeshwa ni ukombozi kwa familia na Taifa kwa ujumla.

“Ukiwekeza kwa Mwanamke hutopoteza kitu chochote, hivyo Shirika hili nalipongeza sana na Serikali ipo pamoja na nyie, kwa kuhakikisha Mwanamke anakombolewa kiuchumi,”alisema Telezia.

Aidha, alitumia pia fursa hiyo kutoa wito kwa wanawake Wajasiriamali, kwamba wasije wakajiingiza kwenye mikopo kausha damu, bali watumie fursa ya Mikopo ya Halmashauri Asilimia 10 ambayo itaanza kutolewa hivi karibuni.

Mmoja wa wanawake Wajasiriamali ambaye amenufaika na Mafunzo ya utengenezaji wa Sabuni kutoka TYC Elizabeth William, ameshukuru kujengewa uwezo wa kuzalisha Sabuni na sasa yupo vizuri kiuchumi.