TVLA: Tuna teknolojia kukabiliana na magonjwa ya wanyama kwa kutumia vina saba

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 04:00 PM Jul 06 2024
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dk. Stella Bitanyi (kushoto) akitoa elimu kwa mdau wa Mifugo kuhusiana uchunguzi wa magonjwa ya minyoo inayoathiri afya za Mifugo ili kuweza kuitambua na kushauri dawa zinaweza kutibu minyoo
Picha: Mpigapicha Wetu
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) Dk. Stella Bitanyi (kushoto) akitoa elimu kwa mdau wa Mifugo kuhusiana uchunguzi wa magonjwa ya minyoo inayoathiri afya za Mifugo ili kuweza kuitambua na kushauri dawa zinaweza kutibu minyoo

WAKALA wa Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), ina teknolojia mbalimbali za kitaalam kukabiliana na magonjwa ya wanyama ikiwemo ya kutumia vina saba ambapo mnyama huchukuliwa sampuli na kupimwa ili kujua aina ya ugonjwa unaomsumbua.

Teknolojia hiyo ni miongoni mwa zinazotolewa na TVLA ambazo zinasaidia kufanya utambuzi wa magonjwa yote ya wanyama  kwa lengo la kujua aina ya magonjwa yanayowasumbua na kutoa dawa stahiki.

Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dk. Stella Bitanyi akizungumza kwenye maonesho ya Biashara ya Kimataifa yanayofanyika jijini Dar es Salaam, amesema  lengo lao ni kubuni na kutumia  teknolojia mbalimbali kwa ajili ya kuhudumia wanyama.

“ Lengo la kubuni teknolojia hizi ni kusaidia mifugo yetu isipate madhara  yeyote, uvumbuzi wetu unalenga kutatua matatizo  ya kiafya yanayoikumbuka mifugo, ni muhimu wadau wa ufugaji wakafika katika banda letu kujifunza masuala mbalimbali kuhusu maabara yetu,” amesema Dk. Stella.

Ameongeza katika maonesho hayo wanatoa elimu 
kuhusu umuhimu wa uchanjaji wa mifugo, utambuzi wa magonjwa ya wanyama, uhakiki wa ubora wa vyakula vya Mifugo, utafiti wa magonjwa ya wanyama na ushauri kuhusu matumizi sahihi ya dawa za mifugo.

Aidha TVLA inatoa elimu ya udhibiti wa wadudu aina ya mbung’o pamoja na kuwadhibiti wadudu hao ambao hueneza ugonjwa wa Nagana pamoja  kudhibiti magonjwa yaenezwayo na kupe kama ndigana kali na ndigana baridi kwa kuhakiki ubora wa viuatilifu kwa ajili ya kuogesha wanyama ili kudhibiti kupe.


Baadhi ya wadau wa Mifugo waliotembelea banda la TVLA wamefurahishwa na huduma zinazotolewa hasa elimu ya uchunguzi wa magonjwa ya Mifugo  kabla ya kuwatibu pamoja na elimu ya uchanjaji wa mifugo kwani walikuwa wanachanja Mifugo yao bili kuipima kitu ambacho kilikuwa kinasabasha vifo kwa Mifugo yao.

Maonesho ya 48 ya Biashara Kimataifa ya Dar Es Salaam (Sabasaba) yanayokutanisha wafugaji, wakulima, wafanyabishara na wajasiriamali kutoka nchi mbalimbali duniani, na  TVLA imeshiriki kwa kuonesha teknolojia mbalimbali za kitaalamu na za kiubunifu.