RUWASA yaagizwa kuziwezesha jumuiya za maji

By Thobias Mwanakatwe , Nipashe
Published at 03:08 PM Jul 06 2024
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava (aliyevaa skafu).
PICHA: Thobias Mwanakatwe
KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava (aliyevaa skafu).

KIONGOZI wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Godfrey Mnzava, ameiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijiji (RUWASA), kuweka utaratibu wa kuziwezesha Jumuiya za Watumia Maji kifedha na mafunzo ili ziwe kutunza vizuri raslimali maji na miundombinu na hivyo kudumu muda mrefu kutoa huduma za maji kwa wananchi kwa kiwango bora.

Ametoa agizo hilo leo (Julai 6, 2024) wakati wa kuzindua mradi wa maji katika kijiji cha Mabondeni Halmashauri ya Itigi wilayani Manyoni Mkoani Singida ambao umegharimu Sh.milioni 280 ambao utahudumia zaidi ya wananchi 2500.

Mnzava amesema serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kujenga miradi ya maji ili kuwawezesha wananchi kupata huduma ya maji safi na salama hivyo miundombinu ya miradi hiyo inatakiwa kutunza vizuri ili iendelee kutoa huduma hizo na jukumu hilo linapaswa kufanywa na Jumuiya za Watumia Maji.

Amesema pia wananchi wanapaswa kutunza vyanzo vya maji visiharibiwe kwani vyanzo vya maji vikiwepo vitaongeza upatikanaji wa maji na hivyo kuondoa kero ya upatikanaji wa maji kwa wananchi kama ilivyo dhamira ya rais Samia Suluhu Hassan ya kusogeza huduma za maji kwa karibu kwa wananchi.

Aidha, Mnzava ambaye aliridhia mradi huo na kuuzindua ameipongeza RUWASA kwa kutekeleza vyema mifumo ya manunuzi ya umma hali ambayo imesaidia kupunguza malalamiko kwamba wapo baadhi ya wakandarasi wanapendelewa kupewa zabuni za kujenga miradi ya maji.