Kairuki ahimiza Watanzania kujifunza asili, urithi wao 77

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 06:00 PM Jul 06 2024
Waziri wa Maliasili na Utalii, Angelah Kairuki, akizungumza na wajasiliamali alipotembelea Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.
PIcha: Na mwandishi wetu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Angelah Kairuki, akizungumza na wajasiliamali alipotembelea Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Angelah Kairuki, amesema ni muhimu kila Mtanzania kufahamu asili na urithi wao ili kudumisha mila na desturi kwa kutembelea vivutio vya utalii.

Amesema wizara hiyo ina vivutio vingi vya utalii hivyo wananchi wanaotembelea Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) watumie fursa ya kutembelea kwenye banda lao.

Waziri Kairuki ametoa kauli hiyo, jana wakati akitembelea mabanda mbalimbali taasisi zilizochini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ikiwamo Bodi ya Utalii TTB katika maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.

Waziri Kairuki amesema kuwa ni vyema jamii ikatumia fursa ya uwapo wa maonyesho hayo kujifunza na kujionea masuala mbalimbali ya utalii ili kujiongezea utamaduni wa kujua historia ya nchi yao.

"Ni umuhimu kutumia fursa mbalimbali zinazotokana na mwingiliano wa Taasisi za Serikali zilizopo na kampuni binafsi zinazoshiriki kwenye maonesho hayo kwa lengo la kukuza uhusiano utakaoleta tija," amesema Kairuki.

Aidha Waziri Kairuki ametoa rai kwa wazazi wenye wanafunzi waliohitimu kidato cha nne kutembelea banda la Wizara ya Maliasili na Utalii na kuzungumza na wataalamu katika vyuo vilivyo chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii kama Chuo cha Misitu Olmotonyi, Chuo cha Viwanda vya Misitu (FITI), Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori (MWEKA), Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT) na vyuo vingine ili kujua fursa mbalimbali za kujiunga na vyuo hivyo.

Ofisa Utamaduni kutoka Makumbusho ya Taifa la Tanzania,Chance Ezekiel amemweleza Kairuki baada ya kutembelea banda lao kuwa, lengo la makumbusho hiyo ni kuhakikisha wanawajulisha Watanzania umuhimu wa kuenzi na kupenda urithi wao.