Wasichana 164 waliokatishwa masomo wapata elimu ya ufundi

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 01:26 PM Jul 06 2024
Binti Queen Maige (21) akionyesha namna ya kushona nguo wakati wa mahafari ya 21 ya chuo cha ufundi Mwakata (SFS) yaliyofanyika kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga.
PICHA: SHABAN NJIA
Binti Queen Maige (21) akionyesha namna ya kushona nguo wakati wa mahafari ya 21 ya chuo cha ufundi Mwakata (SFS) yaliyofanyika kata ya Mwakata Halmashauri ya Msalala mkoani Shinyanga.

WASICHANA 164 waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali ikimemo ndoa na mimba za utotoni, wamehitimu mafunzo ya ufundi stadi ambayo yatawasaidia kujikwamua kiuchumi na kuondokana na utegemezi.

Aidha stadi walizopata zitawawezesha kujikita zaidi katika kazi, lakini pia kuondokana na vishawisha vya mapenzi yasiyo salama.

Imeelezwa kuwa Shirika lisilo la kiserikali la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF) ndilo lililofadhiri masomo ya wasichana hao, kupitia mradi wa ‘chaguo langu haki yangu’ unaotekelezwa katika mikoa ya Shinyanga na Mara, katika chuo cha ufundi Mwakata (SFS).

Mratibu wa mradi huo Joyce Kessy amesema shirika liliwafadhiri wasichana 164 waliokatisha masomo yao kwa sababu mbalimbali ikiwemo, ndoa ya utotoni, mazingira magumu, mimba na kukeketwa, ili wapate ujuzi utakaowasadia kuendesha maisha yao na hivyo kutokuwa tegemezi kwenye jamii.

Amesema, kati ya hao 45 wanatoka Musoma mkoani Mara, Kishapu 75 na Kahama 44 na wanajipanga kuwapatia vifaa vya kazi ili kuendeleza ujuzi wao walioupata na kuwataka kuchangamkia mikopo ya asilimia 10 isiyokuwa na riba ili kupata mitaji.

Mkuu wa chuo hicho, Padri John Denisi amesema, jumla ya wanachuo 301 wamehitimu kati yao 164 ni wale waliofadhiriwa masomo na Shirika la Wildaf na wamejifunza Ufundi umeme, Ushonaji, Magari, Bomba, Sekretari, Komputa pamoja na Saluni na Mapambo.

Akizungumza kwa niaba ya mabinti hao Queen Maige amesema, alihitimu elimu yake ya msingi mwaka 2015 katika shule ya msingi Kinyalili Butiama na mwaka uliofuata wa 2016 mjomba wake ambaye hakumtaja jina, alimlaza kuolewa kwa mahali ya ng’ombe sita.

Amesema, elimu aliyoipata itamsaidia kuendesha familia yake na kutojihusisha katika vitendo vya kuuza mwili wake, na kwamba licha ya kuwa na ndoto ya kuwa Mwanajeshi lakini sasa amekuwa fundi cherehani na anajiandaa kujiajiri ili aweze kulea watoto wake wawili pamoja na mama yake.