Fei Toto ang'ara, atamba heshima Azam FC itarejea

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 07:38 AM Oct 05 2024
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto'
Picha: Mtandao
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto'

KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' amefikisha pasi nne za mabao katika michezo ya Ligi Kuu Bara na kuisaidia timu yake kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Namungo, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi hapo juzi.

Fei Toto alipiga kona dakika ya 76 ambayo ilitua kichwani kwa Lusajo Mwaikenda na kuipatia Azam FC bao pekee kwenye mechi hiyo ya raundi ya saba.

Baada ya mechi kumalizika, Fei Toto aliwaambia mashabiki wa Azam kuwa na subira, akiahidi watarejea katika ubora uliozoeleka.

Kiungo huyo alisema wanaendelea kuimarika na wanatakiwa kuwa wavumilivu kwa sababu bado mwalimu wao ni mgeni, na amekuwa akifanya kazi kubwa.

"Mchezo ulikuwa mgumu kwetu, tumekosa ushindi michezo miwili iliyopita, mmoja tumefungwa na mmoja tukatoka sare, unajua mwalimu ni mpya, tunaendelea kufuata maelekezo yake kidogo kidogo, na waambia mashabiki wa Azam wasikate tamaa timu itakaa sawa," Fei Toto alisema.

Aliongeza si lazima yeye kufunga kama anaona hayupo kwenye eneo sahihi la kufanya hivyo, badala yake anachoangalia ni kuisaidia timu yake.

"Sijafunga bao lolote mpaka sasa, lakini ujue kufunga bao huwa inatokea kama unakaa sehemu sahihi, siyo unajiamulia tu, kama uko eneo la kutoa pasi basi inabidi utoe siyo kulazimisha kufunga, kwanza tunaangalia timu," alisema nyota huyo.

Ushindi huo unaifanya Azam kufikisha pointi 12 kwa michezo saba iliyocheza, ikishinda mechi tatu, sare tatu na kupoteza moja, ikiwa kwenye nafasi ya tano.

Ulikuwa ni ushindi wa kwanza kwa Azam baada ya michezo miwili, ilipopoteza kwa mabao 2-0 dhidi ya Simba na Jumapili iliyopita ililazimishwa suluhu ugenini dhidi ya Mashujaa FC.

Kiungo huyo wa zamani wa Yanga, aliyemaliza Ligi Kuu msimu uliopita akiwa na 'asisti' saba, hajafunga bao lolote mpaka sasa, hata hivyo msimu uliomalizika alimaliza katika nafasi ya pili akiwa na magoli 19, akipitwa mabao mawili tu na mshindi wa kiatu cha dhahabu, Stephane Aziz Ki wa Yanga.

Baada ya kupoteza, Namungo inasalia na pointi zake sita, ikiwa imecheza michezo sita, nafasi yake ikiwa ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu.