Mahakama ya Mafisadi yaamuru nyumba, fedha na gari vitaifishwe

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 11:42 AM Oct 04 2024
Mahakama ya Mafisadi
Picha:Mtandao
Mahakama ya Mafisadi

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, maarufu Mahakama ya Mafisadi, imemtia hatiani mfanyabiashara Oje Boniface, raia wa Nigeria na kumuhukumu kifungo cha miaka tisa gerezani na kuamuru nyumba, gari na fedha zitaifishwe na serikali.

Hukumu hiyo ya mahakama ilisomwa juzi mbele ya Jaji Godfrey Isaya baada ya mshtakiwa kupitia Wakili wake Lovenes Ngowi kukiri kosa.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Issaya alisema mshtakiwa aliingia maridhiano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kukiri kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya cocaine gramu 420.33.

"Kukiri kosa ni sehemu ya maridhiano, pande zote mbili ziliomba ziongozwe na mkataba wa maridhiano.

"Mahakama inabidi kufuata maridhiano kwa kuwa sehemu ya makubaliano mshtakiwa atumikie kifungo cha miaka 12 badala ya miaka 30 au maisha na kwamba katika kutoa adhabu hiyo miaka mitatu aliyokaa ndani izingatiwe.

"Mahakama inapunguza miaka mitatu, hivyo mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka tisa jela," alisema Jaji Isaya.

Alisema mahakama inatoa amri dawa za kulevya gramu 316.40 na gramu 103.93 ziharibiwe kwa kuchomwa moto.

"Kipande cha ardhi chenye nyumba iliyoko maeneo ya Mbezi Makabe, gari lenye namba ya usajili T 414 DQF Toyota Premium zinataifishwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania," alisema.

Jaji Isaya alisema mshtakiwa anatakiwa kuzingatia vigezo vyote vilivyoko katika mkataba na ana haki ya kukata rufani kwa adhabu peke yake.

Katika kesi hiyo, Jamhuri iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Martietha Magata, aliyedai kuwa mshtakiwa alikuwa anakabiliwa na shtaka moja la kujihusisha na biashara haramu ya kusafirisha dawa za kulevya.

Alidai kuwa mshtakiwa alikamatwa Mei 24, 2021 akiwa na dawa za kulevya aina cocaine gramu 316.40 ndani ya gari na alipokwenda kupekuliwa nyumbani kwake Mbezi Makabe, wilayani Ubungo, alikutwa na gramu 103.93.

Mshtakiwa aliposomewa maelezo ya awali, alikiri kukutwa na dawa hizo na kwamba wakati anakamatwa alikuwa na umri wa miaka 32.

Mshtakiwa pia alikiri kukutwa na fedha taslimu Sh. 310,000, fedha za Malawi 7,200, fedha za Kenya Sh. 50 pamoja na dawa za kulevya ambapo vyote kwa pamoja na mkataba wa mauziano ya ardhi na kadi ya gari vilitolewa mahakamani kama vielelezo namba moja na pili.

Mahakama iliamuru dawa zifunguliwe na zilifunguliwa, mshtakiwa na wasikilizaji walishuhudia zikiwa katika muundo wa mipira midogo minne.

Baada ya kutiwa hatiani, upande wa Jamhuri uliomba amri ya kuharibiwa dawa, pia ukaomba nyumba, gari na fedha zitaifishwe kuwa mali ya serikali.

Wakili Marietha alidai Jamhuri inaamini fedha zilitokana na mazalia ya biashara haramu ya dawa za kulevya.

Wakili Lovenes Ngowi, akimtetea mshtakiwa apunguziwe adhabu, alidai ni mkosaji wa mara ya kwanza, familia inamtegemea, ana watoto watatu na mke na kutokana na makubaliano aliyoingia, familia haina nyumba ya kuishi.

Aliomba mahakama impunguzie adhabu, impe kifungo cha muda mfupi ili akae kidogo gerezani arudi kuhudumia familia yake.

Mahakama ilizingatia hoja zote, ilimtia hatiani na kumhukumu kwenda jela miaka tisa na mali zake ambazo ni nyumba, gari na fedha alizokutwa nazo zinataifishwa na serikali.

Dawa alizokutwa nazo zitahifadhiwa kusubiri utekelezaji amri ya kuziharibu kwa kuzichoma moto.