HII ni sehemu ya pili ya ripoti inayoangazia madhila wanayopata madereva wa vyombo vya moto vinavyotumia gesi mkoani Dar es Salaam.
Katika sehemu ya kwanza jana, kulikuwa na ushuhuda wa adha wanazopata madereva hao, hata kukaa kwenye foleni ya kujaza gesi kwa saa nane. Endelea...
Kaimu Mkurugenzi wa Biashara ya Gesi na Mafuta wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Emmanuel Gilbert, anasema mkakati uliopo unajumuisha ujenzi wa vituo vingine vidogo mkoani Morogoro na vingine viwili mkoani Dodoma, ambavyo vitakamilika ndani ya miezi sita hadi saba kuanzia mwezi uliopita.
Anasema kuwa kwa sasa tayari kuna kampuni 31 ambazo zimeshapata kibali kutoka TPDC na ziko kwenye hatua mbalimbali za kupata ridhaa kutoka kwa msimamizi wa sekta.
Anasema baada ya kuwapatia idhini ya kuwekeza, wanakwenda Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) kupitishwa katika mchakato wa ujenzi ili vituo vijengwe kwa usalama na viwango vinavyotakiwa.
"Kuna kampuni kadhaa ziko kwenye mchakato huo, ndani ya mwaka 2024/25 tunategemea kuwa na vituo vipya 14, ukiachana na hivi vilivyopo. Kati ya vituo hivyo 14, vya TPDC vitakuwa saba na vingine ni kutoka kampuni binafsi.
"Kwa mwaka 2025/26 tunategemea kuwa na vituo 14 tena. Kati yake, vitano vitakuwa vya TPDC na tisa vya kampuni binafsi. Mwaka 2026/27, kutakuwa na vituo vingine 19. Kati yake, vinane vitakuwa vya TPDC na vingine vitakuwa vya kampuni binafsi.
"Kwa hiyo, unaweza ukaona mwanga umeanza kuonekana, uwekezaji kwenye gesi asilia kwa ajili ya magari ni huduma inayopanuka na inaweza kuja kuwa kubwa kuliko ya mafuta. Gesi inauzwa bei rahisi kuliko mafuta," Gilbert anasema.
Ofisa huyo wa TPDC anasema lengo la serikali ni kuhakikisha itakapofika 2030, mwaka ambao ni ukomo wa upimaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu, walau asilimia 80 ya Watanzania wote wenye vyombo vya moto wawe wanatumia nishati safi kuendesha vyombo vyao.
"Gesi ni fursa, gharama ya ununuzi wa mafuta kwa sasa lita moja ni Sh. 3,300 wakati bei ya gesi kilo moja inauzwa Sh. 1,550. Matumizi ya gesi pia yanasaidia kutunza mazingira kwa sababu gesi haitoi moshi," anasema.
Gilbert anasema baadhi ya nchi zimepiga marufuku matumizi ya vyombo vya moto vinavyotumia mafuta, akitolea mfano magari ya kusambaza bidhaa kwenye maduka mijini, magari ya wanafunzi na taxi.
"Wote hao wanalazimishwa kama hawatumii gesi asilia, hawawezi kupata kibali, hivyo na sisi tunafikiria tutafika huko tutakapokuwa tumepata vituo vingi vya kutoa huduma. Hivi sasa tukiweka masharti hayo, maana yake tutaua ajira hizo," Gilbert anahitimisha ufafanuzi wake.
Kukabiliana na uhaba wa vituo vya kujaza gesi nchini, Meneja Mawasiliano na Uhusiano wa EWURA, Titus Kaguo, anasema yamefanyika marekebisho ya sheria, wakitoa rukhsa vituo vyote vya mafuta zaidi ya 2,000 nchini vinaweza kuwekwa huduma ya kujaza gesi.
Anasema taratibu za kisheria zimerekebishwa ili kuwezesha kituo cha mafuta kuwa na miundombinu ya gesi, akibainisha kuwa tayari wamepokea maombi ya kampuni zinazotaka kuwa na huduma hiyo katika vituo vyake vya mafuta.
Kaguo anasema vigezo vya kufungua kituo cha kuuzia gesi, ni sawa na vinavyotumika kufungua kituo cha mafuta huku akiunga mkono hoja kwamba, vituo hivyo vikitapakaa nchi nzima, vitasaidia kufikia adhima ya kupunguza uchafuzi wa mazingira kupitia nishati chafu.
Changamoto ya uhaba wa vituo vya gesi inafahamika kwa Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Felchesmi Mramba. Anawatoa hofu watumiaji wa nishati hiyo kwamba serikali inafanyia kazi suala hilo.
Anasema upatikanaji wa uhakika wa gesi asilia kwa ajili ya vyombo vya moto utawarahisishia wafanyabiashara na wakulima usafirishaji mizigo yao kwa gharama ndogo na kupata faida kubwa.
Watafiti wanabainisha kuwa moshi unaotolewa na magari una hewa ya kaboni monoksaidi, nitrojeni oksaidi na kemikali nyinginezo ambazo zimethibitishwa kusababisha maradhi mbalimbali, ikiwamo saratani.
Ripoti iliyotolewa Februari mwaka huu na Baraza la Kimataifa la Usafiri Salama (ICCT) inaonesha kuwa watu 385,000 walifariki dunia kutokana na moshi unaotolewa na magari kote duniani mnamo mwaka 2015.
Ripoti hiyo inafafanua zaidi kwamba magari yanayotumia dizeli yalichangia zaidi vifo hivyo, yakitajwa kuchangia asilimia 66 ya madhara hayo.
Watafiti hao wanataja mataifa ya Ufaransa, Ujerumani, Italia na India kuwa na magari mengi yanayotumia dizeli, wakibainisha kuwa sekta ya usafiri huchangia asilimia 11 ya vifo vyote vinavyotokana na hewa chafu duniani.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watu 114,000 walifariki dunia China kutokana na moshi unaotokana na magari mnamo mwaka 2015 huku watu 22,000 wakiaga dunia Marekani kutokana na tatizo hilo.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Dk. Immaculate Semesi, anasema uhaba wa vituo vya kujazia gesi ni kikwazo katika kufikia adhima ya kuwa na mazingira safi nchini.
"Ule moshi unaotokana na vyombo vya moto hutengeneza kitu kama blanketi fulani angani, matokeo yake ndio huwa unaona kuna wakati kuna joto la kupitiliza, mvua za kupitiliza au ukame.
"Mabadiliko ya namna hiyo ndio yanasababisha madhara kwa mazingira na binadamu wakati mwingine yanaathiri afya kwa kuzalisha mbu wengi, magonjwa ya mlipuko, kukosekana kwa malisho, mafuriko, mmomonyoko wa udongo na mavuno hafifu kwa sababu mabadiliko ya tabianchi huja na mambo mengi," anasema.
Kwa kuzingatia madhara hayo, mkurugenzi huyo anasema kuwa mara zote wamekuwa wanahimiza wamiliki wa vyombo vya moto kutumia gesi asilia ili kupunguza athari za kimazingira.
Dk. Immaculate, akieleza kuvutiwa na mwamko wa wananchi kutumia gesi katika vyombo vya moto, anashauri serikali na sekta binafsi kuweka nguvu ya pamoja kuongeza vituo vya gesi ili kupunguza msongamano wa magari na bajaji kwenye vituo vichache vya kujazia gesi vilivyoko.
Kero ya uhaba wa vituo vya gesi ilishafikishwa mezani kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ambaye hatua za awali alizochukua ni pamoja na kuitaka EWURA kuwezesha ujenzi wa vituo vingi zaidi nchini.
"Tujenge vituo vingi hapa Dar es Salaam, magari ya mafuta ni mengi sana, tukipunguza hiyo volume (kiwango) ya mafuta, magari yakatumia gesi, gharama ya uendeshaji hayo magari itapungua.
"Huu ni mpango wa muda mrefu ambao tutaendelea kuwa nao. EWURA lazima wauchukue kwa kasi kubwa ili utupe matokeo mazuri," anaagiza Dk. Biteko.
Wakati wa Mkutano wa 11 wa Wawakilishi wa Kudumu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) jijini Nairobi, Kenya Julai mwaka huu, wawakilishi Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda na Burundi walikubaliana nchi zao kutunga sheria zitakazohakikisha magari yanayoingizwa ukanda wa Afrika Mashariki yana teknolojia inayosafisha moshi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED