TAWA yatangaza fursa za uwekezaji 77

By Mary Geofrey , Nipashe
Published at 06:08 PM Jul 06 2024
Baadhi ya wananchi wakiendelea kupata maelezo kutoka kwa Ofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendele katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.
Picha: Mpigapicha Wetu
Baadhi ya wananchi wakiendelea kupata maelezo kutoka kwa Ofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) katika Maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba) yanayoendele katika viwanja vya Mwalimu Nyerere.

MAMLAKA ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imetumia Maonesho ya 48 ya kimataifa ya kibiashara yanayoendelea Jijini Dar es Salaam kuhamasisha Watanzania, wawekezaji na wageni kutoka mataifa mengine kuwekeza katika maeneo inayoyasimamia.

Akizungumza na wageni waliotembelea banda la TAWA lililopo ndani ya banda la Wizara ya Maliasili na Utalii Ofisa uUtalii, Daud Tesha, amesema TAWA ina uwanda mpana wa fursa za uwekezaji unaotoa mwanya kwa wawekezaji wa aina mbalimbali kuwekeza katika taasisi hiyo.

 Tesha amesema yapo maeneo mengi yanayohitaji wawekezaji na uwekezaji katika taasisi hiyo kama vile maeneo ya utalii wa picha kwenye maeneo ya hifadhi za wanyamapori, maeneo ya kihistoria yenye utalii wa kiutamaduni, eneo la uwekezaji mahiri.

"TAWA imetenga maeneo kadhaa kwaajili ya kufanyika shughuli za utalii wa picha kutokana na ikolojia na aina ya vivutio vilivyopo katika maeneo hayo ikiwamo Pori la Akiba Mpanga/Kipengere eneo ambalo lina maporomoko ya maji zaidi ya 10 ambayo hutoa burudani safi kwa watalii," amesema Tesha.

"Maeneo  mengine ni Pori  la Akiba Wamimbiki, Tabora ZOO, Ruhila ZOO , Makuyuni Wildlife Park ambapo wananchi wanakaribishwa kuwekeza kwenye miundombinu ya Utalii ikiwemo kujenga Kambi za Kulala wageni (Campsites), Hosteli, Loji na maeneo ya mapumziko mafupi kwa watalii (Picnic Sites)," ameongeza.

Naye Ofisa Habari wa TAWA, Beatus Maganja amekaribisha wananchi wote kutembelea banda la TAWA Ili kupata maelezo ya fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo katika taasisi hiyo.

"Kama kauli mbiu ya Maonesho haya inavyosema kuwa Tanzania ni Mahali Sahihi pa Biashara na Uwekezaji, nitumie fursa hii kuwaambia watanzania wote kuwa TAWA ni Taasisi sahihi kwa biashara na uwekezaji kwani inatoa fursa za uwekezaji wa aina mbalimbali kama vile ujenzi wa loji, kumbi za mikutano katika maeneo yetu, kambi za watalii, michezo ya watoto lakini kama haitoshi mwekezaji anaweza akatumia fursa ya kuwekeza katika mashamba ya wanyamapori, bustani za wanyamapori," amesema Maganja.

Maonesho haya yenye Kauli Mbiu "Tanzania ni Mahali Salama Pa Biashara na Uwekezaji" yameanza Juni 28, 2024 na yanatarajiwa kufikia tamati Julai 13, 2024.