Jela miaka minne kwa kumkata viganja mamake mdogo

By Daniel Limbe , Nipashe
Published at 12:47 PM Jul 06 2024
Monica Laurent Nonga, aliyekatwa vigacha vyake, akiwa mahakamani,
PICHA: Daniel Limbe
Monica Laurent Nonga, aliyekatwa vigacha vyake, akiwa mahakamani,

MKAZI wa Kijiji cha Bwanga, wilayani Chato, Mkoa wa Geita, Faida Enocka, amehukumiwa kifungo cha miaka minne jela na kulipa fidia ya shilingi milioni 3, baada ya kukutwa na hatia ya kumkata na kumjeruhi, Monica Laurent Nonga, mkazi wa Kijiji cha Butobela Buseresere wilayani humo, hali iliyosababisha kuondoa viganja vya mikono yake kutokana na imani za kishirikina.

Hukumu hiyo imetolewa na Mahakama ya Wilaya ya Chato kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na pande mbili kati ya mwendesha mashitaka wa Jamhuri, na mshitakiwa katika kesi hiyo namba 757 ya mwaka 2023, ambapo baada ya kujiridhisha pasipo shaka mahakama ikafikia uamuzi huo.

Awali mwendesha mashitaka wa Jamhuri, Mauzi Lyawatwa, ameiomba mahakama hiyo kutenda haki kwa kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa huyo ikiwa ni pamoja na kumlipa fidia, Monica kutokana na ukatili wa kinyama aliomtendea na kumsababishia kuwa tegemezi kwa watu wengine baada ya kuondolewa viganja vyake.

Akisoma hukumu, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Erick Kagimbo, amesema kwa kuzingatia ushahidi uliowasilishwa na pande zote ikiwemo mshitakiwa mwenyewe, ni wazi kuwa mahakama imejiridhisha pasipo shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 225 cha sheria ya makosa ya jinai sura ya 16 Kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Na kwamba kutokana na hali hiyo,mshitakiwa atatakiwa kutumikia kifungo cha miaka minne jela na kulipa fidia ya shilingi milioni tatu, ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo, huku mahakama hiyo ikimpa mashitakiwa haki ya kukata rufaa iwapo atakuwa hajaridhika na adhabu iliyotolewa.