TAHA, Tanga kuimarisha kilimo cha viungo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:34 AM Jul 04 2024
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi Kilele ya Kilimo cha Maua, Mboga, Matunda na Viungo (TAHA), Dk. Jacqueline Mkindi (kushoto)  na Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Tanga, Dk. Frederic Sagamiko, wakionyesha makabrasha baada ya kutiliana saini.
Picha: Mpigapicha Wetu
Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi Kilele ya Kilimo cha Maua, Mboga, Matunda na Viungo (TAHA), Dk. Jacqueline Mkindi (kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Tanga, Dk. Frederic Sagamiko, wakionyesha makabrasha baada ya kutiliana saini.

HALMASHAURI ya Jiji la Tanga imetia saini makubaliano na Asasi kilele inayojishughulisha na kilimo cha mboga, maua, matunda na viungo nchini (TAHA) kwa ajili ya kubadili kilimo hicho na kuwa cha kibiashara.

Makubaliano hayo yalisainiwa Julai 2, mwaka huu na watendaji wakuu wa taasisi hizo mbili, Dk. Jacqueline Mkindi wa TAHA na Dk. Fredreck Sagamiko wa Jiji la Tanga, makao makuu ya TAHA, jijini Arusha.

Makubaliano hayo yameainisha ujenzi wa ghala ambalo litatumika kuongeza thamani na kuhifadhi viungo katika jiji hilo, kwa ajili ya kusafirisha masoko ya nje.

“Lengo kuu la makubaliano yetu ni kubadilisha kilimo cha viungo kuwa cha kibiashara ili kutengeneza ajira za kinamama, vijana na wenye ulemavu katika Jiji la Tanga,” Dk. Sagamiko alisema baada ya kutia saini makubaliano hayo.

Alisema wamechagua kushirikiana na TAHA kutokana na uwezo wa kitaalam na uzoefu wake katika kuendeleza kilimo cha viungo, utalaamu wa kisasa wa kuhifadhi zao hilo, kuongeza thamani na kuwaunganisha wakulima na masoko ya nje.

Alibainisha kwamba kilimo cha viungo kimekuwa kikifanyika Tanga tangu enzi za mababu, lakini hakijawahi kuwa na manufaa makubwa kwa sababu kinaendeshwa kienyeji.

“Tumeona ni wakati mwafaka kuwasaidia wakulima wa Tanga kubadilisha kilimo hicho na kuwa cha kibiashara, ili waweze kunufaika na jasho lao, lakini pia kuchangamsha uchumi wa Jiji la Tanga,” alisisitiza Dk. Sagamiko.

Kwa kuanzia, halmashauri hiyo imetenga eneo la ekari tano kwa ajili ya ujenzi wa ghala hilo la kisasa ambalo litatumika kwa shughuli za kusindika na kuhifadhi viungo kabla ya kusafirishwa kwenda katika masoko ya nje.

Dk. Sagamiko alisema pia halmashauri yake imetenga shamba la ekari 100 ambazo zitatumika kwa kilimo cha kisasa cha viungo, ili liwe kama shamba darasa kwa wakulima wa viungo kutoka sehemu mbalimbali.

Mkurungezi huyo na timu yake inaamini kuwa utekelezaji wa makubaliano hayo utakapoanza, utapeleka mapinduzi makubwa ya kilimo cha viungo sio tu kwa jiji hilo, bali na maeneo mengine.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo, TAHA itapaswa kusaidia katika maeneo ya kitaalamu kwa kuhakikisha ghala hilo linapata ithibati zote za kimataifa kwa ajili ya kuhifadhia viungo vinavyosafirishwa katika masoko ya ng’ambo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Mkindi alisema TAHA kupitia Mradi wa Tuhifadhi Chakula unaofadhiliwa na Shirika la Misaada la Kimataifa la Marekani la USAID, itasaidia jiji la Tanga kwenye suala la kupunguza uharibifu wa viungo baada ya mavuno. 

Mradi wa Tuhifadhi Chakula ni mpango wa kimkakati wa mageuzi wa miaka mitano, unaochochewa na uwekezaji wa Dola za Kimarekani milioni 24 uliofanywa na USAID na TAHA kupewa jukumu adhimu la utekelezaji wa mkakati huu, ili kufuta machozi ya wakulima ambao wamekuwa wakipoteza mazao yao miaka nendarudi.

Lengo la msingi la mradi ni kupunguza upotevu na utupaji wa chakula, mpango huu pia unajitahidi kuimarisha uthabiti wa Tanzania kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi na usalama wa chakula, ukiunga mkono mpango wa awamu ya pili ya Programu ya kitaifa ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo – ASDP II.

“TAHA pia mradi mwingine unaofadhiliwa na SIDA itapeleka wataalamu wa kilimo cha kibiashara kutoa mafunzo kwa wakulima wa viungo katika jiji la Tanga, itapeleka pia wataalamu wengine wa uongezaji wa thamani viungo, watalaamu wengine wa masoko nakadhalika ili kuhakikisha kilimo hicho cha viungo kinakuwa cha kibiashara kweli kweli,” alisisitiza Dk. Mkindi alisisitiza.

Naibu Meya wa Jiji la Tanga, Rehema Mhina alishukuru asasi ya TAHA kwa utayari wao wa kusaidia Halmashauri ya Jiji la Tanga katika adhima yake ya kugeuza kilimo cha viungo kuwa cha kibiashara.

“Niwahakikishie kwamba jiji la Tanga litashirikiana na ninyi kwa dhati kuhakikisha jambo hili linafanikiwa. Tutatumia asilimia kumi ya mapato ya ndani ya jiji kutoa mikopo kwa akina mama, vijana na walemavu waweze kulima kisasa na wanufaike,” alisisitiza Mhina.