Nyusi: Afrika tujitegemee, wakubwa hawatufai tena

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:59 AM Jul 04 2024
Rais Samia Suluhu Hassan na mgeni wake, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi wakimsikiliza Mwenyekiti wa Umoja wa Wadau wa Kahawa wa Sekta Binafsi katika nchi 11 barani Afrika, Amir Esmail (kushoto), kabla ya kufungua Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan na mgeni wake, Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi wakimsikiliza Mwenyekiti wa Umoja wa Wadau wa Kahawa wa Sekta Binafsi katika nchi 11 barani Afrika, Amir Esmail (kushoto), kabla ya kufungua Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa Dar

RAIS wa Msumbiji, Filipe Nyusi, amesema vita vilivyotikisa mataifa mbalimbali duniani pamoja na mlipuko wa UVIKO-19 viwe ni funzo kwa nchi za Tanzania na Msumbiji kutengeneza vitu vyao wenyewe badala ya kuendelea kutegemea kutoka nchi nyingine.

Nyusi alitoa kauli hiyo jana wakati akifungua Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF), yanayofanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere maarufu, Sabasaba.

Alitoa mfano katika vita hivyo vilivyotokea baadhi ya nchi duniani kuwa pamoja na kutokea katika mataifa ya mbali, lakini Tanzania na Msumbiji ni miongoni mwa zilizoathirika.

“Jambo jingine kuhusiana na kuyumba kwa masoko kunakosababishwa na vita huko Ulaya na Mashariki ya Kati ambako vinachelewesha kuondoa hatari ya kupanda kwa bei ya bidhaa za nishati zinazosababisha mfumuko wa bei na gharama kubwa za ufadhili na kuathiri akaunti za umma na huduma za benki katika nchi nyingi hasa Jangwa la Sahara, vinatufundisha tutengeneze vitu kutoka kwetu,” alisema Nyusi.

“Tunaona hata watu wetu wanakosa hili wanakosa lile, kwa hiyo japo tunaona kama viko mbali, lakini vinatusumbua, mfano wanachukua madini yetu wanakwenda kutengeneza huko sasa kama hawatengenezi kutokana na hicho kinachoendelea huko sisi tunaathirika, kwa hiyo pamoja na kwamba tuna matatizo, yanaongezeka zaidi, kwa hiyo ni lazima tujifunze sasa vitu vyetu tuanze kuvifanya huku kwenye nchi zetu,” alisema Nyusi.

Alisema Tanzania na Msumbiji wamejipanga na kushirikiana zaidi kuboresha mazingira ya biashara ikiwamo kuharakisha ukuaji wa uchumi.

“Tunataka kushirikiana katika eneo la sekta ya viwanda, usafiri na huduma zinazojikita katika miji mikubwa pamoja na bidhaa za walaji, utumiaji na uchakataji wa pamoja wa bidhaa ambazo ni za kawaida kwa pande zote mbili ikiwamo korosho, katani na mkongo ili kuongeza kiwango cha ukuaji wa kibiashara. Haya yatashawishi kuundwa kwa sekta ya viwanda na kuchochea utafiti wa kisayansi utakaoleta kipato kwa familia na maendeleo ya nchi.

Alisema mara nyingi wakulima katika nchi hizo wanalima korosho halafu wanauza kwa bei ndogo, lakini zikitoka nje ya nchi hizo inauzwa bei kubwa yenye utofauti. 

Aliwaalika wawekezaji kutoka Tanzania kuchangamkia fursa mbalimbali zilizopo katika nchi ya Msumbiji kwenda kuwekeza.

“Ndugu zangu nasema hivi kwa sababu Msumbiji mtu yeyote anaweza kuwekeza, kwa hiyo kama una fedha zako, chagua ndugu yako wa Msumbiji uje uwekeze, hata kama una lima zao fulani kwa ukubwa zaidi una soko lako kwetu njoo uwekeze, msijifunge Tanzania tu,” alisema Nyusi.

Kadhalika, alisema nchi hiyo ina sekta zake za kimkakati hususani katika kilimo, nishati, miundombinu, viwanda, madini, utalii, kwa sababu nchi yetu iko karibu sana na Tanzania, tupo tayari kukaribisha mipango ya uwekezaji yenye tija kutoka Tanzania katika sekta hizo za kimkakati.

Alisema kuendelea kukua kwa uchumi wa Tanzania kunatokana na kuongezeka kwa imani za kampuni na urari wa biashara bora ambao umechangia kuongoza mahitaji ya jumla.

Alisema Uchumi wa Tanzania ambao unategemea sana madini, utalii, madini kilimo na viwanda unatarajiwa kukua kwa kasi zaidi mwaka huu kuliko mwaka jana kwa kufikia asilimia 5.4 kutoka 5.1 za mwaka jana.

Alisema kuna haja ya nchi hizo mbili kuendelea kuonyesha fursa zao za kiuchumi na bidhaa zao ili kuchochea biashara zaidi na kuhamasisha uwekezaji zaidi ili kuchochea uchumi na maendeleo ya usalama wa chakula, ushindani kati ya kampuni ndogo ndogo na uzalishaji mali, kukuza ajira ili kufikia ustawi wa watu kwenye nchi hizo.

ATANGAZA KUNG`ATUKA

Nyusi alitumia hadhara hiyo kutangaza kwamba hatagombea tena urais wa nchi hiyo na ataheshimu Katiba.

“Nikipewa ruhusa na Rais Samia, dada yangu, ningependa kuwataarifu kuwa nchi yangu ya Msumbiji, itakuwa na uchaguzi mkuu Oktoba 9, mwaka huu, kwa utii wa dhati wa Katiba niliyoiapa kuilinda na kuiheshimu, sitagombea tena urais. Kama Mwalimu Nyerere (Rais wa kwanza Tanzania), nitang`atuka, nawashukuru wananchi wangu kwa kipindi chote hiki walichonipa nafasi kuwaongoza,” alisema Nyusi.

SAMIA APONGEZA

Rais Samia alimpongeza Rais Nyusi kwa kukubali kuwa mgeni rasmi kwenye maonesho na kwamba ni nyenzo katika kuchochea maendeleo ya kibiashara na ukuaji wa sekta mbalimbali za kiuchumi.

Alisema serikali itaendelea kuifanya Tanzania kuwa mahali sahihi na salama kwa uwekezaji na kutoa wito kwa Watanzania kutembelea na kushiriki maonesho hayo makubwa na kutumia vizuri programu zinazoandaliwa katika kupata wadau wa biashara na uwekekezaji.

Alipongeza kampuni 11 ambazo zimeanza kutumia fursa hiyo muhimu kwa kusafirisha bidhaa za kahawa, katani, viungo, karanga na tumbaku kwenda nchi mbalimbali za Afrika ikiwamo Algeria, Misri, Ghana na Morocco.

Alisema serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara nchini.

“Mfanyabiashara yeyote mwenye maoni ya kuboresha, kujenga na kusaidia nchi milango ipo wazi na waendelee kuwasiliana na mamlaka zetu mbalimbali ikiwamo wizara yenye dhamana ya biashara.

Mmoja wa wafanyabiashara na Mwenyekiti wa Umoja wa Wadau wa Kahawa wa Sekta Binafsi katika nchi 11 barani Afrika, Amir Esmail, alisema kwa sasa wanafurahia mazingira ya biashara yaliyowekwa na serikali.

“Biashara kwa sasa ni nzuri sana na nimemshukuru Rais Samia kwa kufungua nchi pamoja na maandalizi mazuri ya mabanda kwenye maonesho ya mwaka huu, haijawahi kutokea mabanda kupendeza zaidi kama ilivyo mwaka huu, tunashukuru na tunapongeza sana,” alisema Nyusi.

* Imeandaliwa na Elizabeth Zaya, Christina Mwakangale na Pilly Kigome