Vigingi viwili vya mrithi wa Kidata TRA hivi hapa

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:06 AM Jul 04 2024
Vigingi viwili vya mrithi wa Kidata TRA hivi hapa.
Picha: Mtandao
Vigingi viwili vya mrithi wa Kidata TRA hivi hapa.

WACHUMI na wafanyabiashara wamezungumzia uteuzi mpya wa Yusuph Mwenda kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), wakitaja mambo mawili yanayomsubiri.

Hayo ni kupanua wigo wa kodi na kubadilisha au kuimarisha dhana nzima ya usimamizi wa kodi nchini.

 Usiku wa kuamkia jana, Ikulu ilitangaza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amefanya mabadiliko ya uongozi katika maeneo kadhaa, akimwondoa Alphayo Kidata katika nafasi ya Kamishna Mkuu wa TRA na kumteua kuwa Mshauri wa Rais Ofisi ya Rais, Ikulu. 

 Nafasi iliyoachwa wazi na Kidata TRA imechukuliwa na Mwenda, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA).

 Mabadiliko hayo yamefanyika ikiwa imepita wiki moja tangu kuitishwe mgomo wa wafanyabiashara katika mikoa mbalimbali nchini, wakilalamikia kuwapo utitiri wa kodi unaotozwa na TRA.

 Vilevile, ni malalamiko yaliyofanywa siku chache baada ya mabalozi 10 wanaowakilisha nchi zao Tanzania, kuwasilisha malalamiko serikalini dhidi ya vikwazo vya uwekezaji wa raia wake nchini, hususani vya kikodi, wakiinyooshea kidole TRA moja kwa moja kuwa kiini cha tatizo.

 Katika mazungumzo na mwandishi wa habari hii jana kuhusu mabadiliko hayo, wachumi na wafanyabiashara walipongeza hatua hiyo, huku wakitaka kuwapo ushirikiano na utatuzi wa changamoto zinazojitokeza ili kuongeza wigo wa walipakodi nchini.  

 Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti na Kupunguza Umaskini nchini (REPOA), Dk. Donald Mmari, alisema jukumu lolote ambalo mtu anakabidhiwa na Rais ni kwa ajili ya wananchi.

 Hivyo, Dk. Mmari alisema linapaswa kufanywa kwa uaminifu na kusikiliza; kama ni kukusanya kodi basi iwe kwa uadilifu na kwa haki.

 "Kusikiliza changamoto za wananchi, kupata ushauri, kusimamia sheria na pale ambapo sheria inaonekana kukinzana na matakwa ya maendeleo ya wananchi, uchukuliwe ushauri wa kubadilisha sheria," alisema.

 Kuhusu changamoto za kimifumo na mabadiliko ya kiuongozi yanayofanywa, Dk. Mmari alisema vyote vinapaswa kutazamwa.

 "Tunafahamu kuna masuala ya kimfumo na sheria. Kama sheria imeelekeza kodi inapaswa kukusanywa na kiwango ni hiki, yanapaswa kutekelezwa kisheria. Lakini sera na sheria ni kitu ambacho kinaweza kuwa na matokeo makubwa zaidi.

 "Kama sheria haikidhi mahitaji ya nchi, wafanyabiashara, wazalishaji shambani na makundi mengine haitajalisha nani anaitekeleza," Dk. Mmari alisema.

 Ushauri wake kwa Kamishna Mkuu mpya TRA, ni kwamba kuna kazi ya kufanya ili kupanua wigo wa kodi, kubadilisha au kuimarisha dhana nzima ya usimamizi wa kodi.

 Alisema suala hilo si jukumu ambalo Kamishna Mkuu wa TRA anaweza kulifanya peke yake, bali yanahitaji mabadiliko ya kimuundo, kimfumo na kisera ambayo yako nje ya kiongozi huyo.

 "Wizara ya Fedha inahusika katika kuangalia sera na sekta nyingine zinazohusika kuangalia namna ya kurasimisha shughuli mbalimbali kama za ufugaji na uvuvi, ili kila anayezalisha apate kipato na kuchangia katika kodi," alisema.

 Dk, Mmari alisema Kamishna Mkuu mpya hana budi kupanua wigo ili kuongeza idadi ya walipakodi nchini na kuongeza kiasi cha kodi kinachokusanywa kulingana na Pato la Taifa ambacho kwa Tanzania kipo chini.

 "Hii si kazi ambayo anaweza kuifanya Kamishna wa mapato peke yake, inahitaji pia kufanyiwa utafiti zaidi, inahitaji kuangalia kama sera inaweza kubadilishwa kidogo na kwa namna gani tunaweza kuimarisha sekta za kiuchumi hususani sekta isiyo rasmi ambayo ni kubwa ili ichangie kwenye mapato, inahitaji ushirikiano wa taasisi nyingi," alisema.

 Kuhusu wafanyabiashara waliofunga maduka na changamoto zinazokabili wawekezaji wa kigeni zilizoainishwa na mabalozi, Dk. Mmari alishauri Kamishna Mkuu mpya akae na kuzichambua ili kuona kiini chake na kuzitafutia ufumbuzi.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Soko Kuu la Kariakoo, Martine Mbwana, alipongeza hatua iliyochukuliwa na Rais Samia, huku akimwomba ushirikiano Kamishna Mkuu mpya ili watatue changamoto zilizopo na kufungua wigo wa watu wengi kulipa kodi.

 "Leo (jana) tumekutana na Kamishna wa Forodha, kubwa tumezungumza kuhusu upokeaji mizigo bandarini na kodi za forodha kwa ujumla wake. Tunaamini Kamishna Mkuu mpya TRA atatupa ushirikiano," alisema.

 Katibu wa Jumuiya hiyo, Justine Beda, alisema, "Tunatamani huyu ndugu yetu Kamishna mpya TRA afuate nyayo za mtangulizi wake aliyeondolewa, tushirikiane kutatua matatizo ya wafanyabiashara ili serikali ipate kodi yake ambayo inalipika.

 "Ingekuwa bora akaangalia mchakato mzima wa malalamiko ya kodi ya wafanyabiashara na walipakodi wengine kwa kukaa na sekta husika na kupatia ufumbuzi," alisema.

 KUHUSU MWENDA

Kamishna Mkuu mpya TRA (Mwenda) aliwahi kuwa diwani wa Mikocheni na Meya wa Kinondoni (2010 hadi 2015).

 Machi Mosi, 2022, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, alimteua kuwa Kamishna wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB), akichukua nafasi ya Salum Yussuf Ali aliyetenguliwa.

Sasa anachukua nafasi ya Kidata ambaye Aprili 4,2021, Rais Samia alimteua kuwa Kamishna Mkuu wa mamlaka hiyo baada ya Machi 25, 2017, kuondolewa kwenye nafasi hiyo na Rais John Magufuli.

Baada ya kutenguliwa TRA, Kidata aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ikulu, nafasi aliohudumu hadi Januari 10, 2018 alipoteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania Canada, akiitumikia kwa miezi 10 hadi Septemba 20, 2019, Rais Magufuli alipomteua kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, nafasi aliohudumu hadi mwaka 2021.

 Taarifa ya Ikulu ya usiku wa kuamkia jana, ilieleza kuwa Rais Samia pia amemteua Dk. Seleman Jafo kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, akibadilishana ofisi na Dk. Ashatu Kijaji anayekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).