RC akemea uadui wakaguzi wa ndani

By Adela Madyane , Nipashe
Published at 09:20 AM Jul 04 2024
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye.

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye, amewataka wafanyakazi wa Halmashauri za Mkoa wa Kigoma kuondokana na kiburi kinachowafanya kuwaona wakaguzi wa ndani maadui.

Andengenye alisema hayo wakati akizungumza na madiwani na wakuu wa idara wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, wakati wa baraza maalum la kuwasilisha hoja 60 za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) za mwaka 2022/23.

Alisema wakaguzi wa ndani ndio wanaoweza kusababisha halmashauri hizo kuondokana na hoja kutoka kwa CAG japo wafanyakazi wengi wamekuwa wakiwaona kama maadui.

“Tuondokane na kiburi na kuwaona wakaguzi wa ndani na wa nje kama si sehemu yetu, wao wamejitolea kutuelekeza na kuboresha mifumo ya fedha ya ndani, tukianza kuwaona kama maadui ndipo tunapoanza kuharibu, wao ni sehemu yetu, tukikaa nao na kushirikiana nao tutaepusha kuwa na hoja nyingi kipindi cha ukaguzi,” alisema Andengenye.

Alizitaka halmashauri hizo kuwawezesha wakaguzi wa ndani kwa vifaa na ujuzi, ili kuongeza ufanisi katika kazi zao huku akiwataka wafanyakazi wengine kufanya matumizi yanayozingatia sheria, kanuni na taratibu za fedha kigezo ambacho kimekuwa kikikiukwa na kusababisha hoja kutokea.

Aidha, aliagiza kuwa ifikapo Julai 31, mwaka huu halmashauri hizo ziwe zimefanyia kazi na kufunga hoja zote zilizoibuliwa na CAG za miaka ya nyuma na za mwaka wa fedha uliopita pamoja na maagizo matano ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC).

Mwakilishi wa Ofisi ya CAG Mkoa Kigoma, Nelson Rwezaura, alisema sababu kubwa ya kuwa na hoja nyingi ni baadhi ya idara kudhani kuwa ukaguzi ni kwa ajili ya idara ya fedha pekee bila kutilia maanani kwamba, idara zinazofanya matumizi zina majibu sahihi juu ya matumizi zaidi ya idara inayofanya malipo.

Aliongeza kuwa watumishi hao wanapaswa kuachana na mtazamo hasi kuwa ukaguzi unalenga kuwaumiza na badala yake waone ukaguzi upo kama kipimo cha kazi na kuupenda, na kwamba wao wanajitahidi kudumisha mahusiano baina yao na wafanyakazi wengine ili kuwa katika muktadha mmoja kwamba lengo la ukaguzi ni kuboresha na kuleta ufanisi katika kazi.

Akiwasilisha hoja za CAG kwenye kikao hicho, Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza, Benedict Kiranda alisema kati ya hoja 31, hoja saba zimefungwa, 22 zipo kwenye utekelezaji na mbili hazijafanyiwa kazi kabisa, huku sehemu kubwa ya hoja hizo zikiangukia katika upungufu wa nyaraka na maelezo yasiyojitosheleza ya matumizi ya fedha na utekelezaji wa shughuli zilizopangwa.

Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Jackson Mateso, alisema wamepokea maelekezo na maagizo yaliyotolewa na kwamba watayafanyia kazi kuhakikisha hoja zinafungwa, lakini wanaweka mikakati ya kuhakikisha halmashauri haizalishi hoja mpya. 

Mateso alisema halmashauri hiyo kwa miaka mitatu mfululizo imepata hati safi na kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 wamefanikiwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa mapato kutoka makadirio ya kupata Sh. bilioni 2.267 na kupata bilioni 3.11 sawa na asilimia 146. 

Alisema halmashauri yake itasimamia sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza utendaji wa halmashauri, ili kuwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa wananchi bila kuwapo ukiukwaji wa taratibu za fedha na utendaji.