Serikali kuboresha zaidi miundombinu Hifadhi za Misitu asilia

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 02:06 PM Jul 03 2024
Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk.Hassan Abas akizungumza n ammoja wa maofisa ya TFS alipotembelea banda lao katika viwanja vya Sabasaba.
Picha: Elizabeth Zaya
Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk.Hassan Abas akizungumza n ammoja wa maofisa ya TFS alipotembelea banda lao katika viwanja vya Sabasaba.

KATIBU Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dk.Hassan Abas amesema serikali imejipanga kuboresha miundombinu katika vivutio mbalimbali kwenye hifadhi za misitu asilia ili kuvutia zaidi watalii katika eneo hilo.

Dk.Abas amesema kwa sasa kuna mwitikio mkubwa wa watalii wa ndani na nje kupendelea kutembelea vivutio vinavyopatikana katika hifadhi hizo asilia za misitu na kwamba serikali imeona fursa katika eneo hilo na imejipanga kuendelea kuiweka katika mazingia ya mvuto zaidi ili yaendelee kutumika kuongeza idadi ya watalii.

Dk.Abas alitoa kauli hiyo alipotembelea Banda la Maliasili na Utalii katika maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF), yanayoendelea katika viwanja vya sabasaba.

Alisema uwapo wa miundombinu bora na madhari nzuri kunawavutia watalii zaidi kupendelea kutumia muda wao mwingi katika misitu hiyo asilia.

Kadhalika, alisema wanaendelea kualika wawekezaji katika hifadhi hizo ikiwamo kujenga maeneo ya kisasa ya kupumzikia watalii, hoteli na huduma nyingine ambazo zitasaidia watalii kupata huduma zote wakati wakifanya utalii katika vivutio hivyo.

“Unajua zamani watu walikuwa wanapendelea zaidi kwenda kufanya utalii wa kuangalia wanyama, lakini tunaona siku hizi mambo yamebadilika, kuna mwamko mkubwa wa kufanya utalii kwenye hifadhi zetu za misitu asilia, kwa mfano tunaona kule Pugu Kazimzumbwi, idadi ya watii inazidi kuongezeka kila siku hata katika hifadhi zetu nyingine za misitu,’alisema Dk.Abas.

“Siku hizi  tunaona watu wanamua kwenda  kupata hewa safi katika maeneo ya misitu yaliyohifadhiwa vizuri, hata kama kuna mambo yake yanamtatiza akienda kule akikaa baadae anatoka yuko vizuri.Kwa hiyo sisi kama serikali tutaendelea kuwekeza na kuiboresha zaidi."

Dk.Abas aliwaalika Watanzania kuwekeza katika ufugaji wa nyuki na uvunaji asali kwa kuwa nalo ni eneo jingine ambalo lina fursa kubwa kwa sasa.

Alisema kutokana na fursa zilizopo katika eneo hilo, serikali imewekeza nguvu zake katika ikiwamo kutoa ruzuku na kuwajengea uwezo wale wenye nia ya kuwekeza katika eneo hilo.

“Kwa hiyo nitoe wito kwa makundi mbalimbali wasisite kuchangamkia fursa zilizopo katika ufugaji wa nyuki na uvunaji wa asali kwa sababu hata soko lake liko vizuri,”alisema Dk.Abas.