Asiyeona afanya utafiti VETA, wenye ulemavu kujiajiri kwa ufundi

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 04:20 PM Jul 03 2024
Rafael Mwambalaswa, akikata akiendelea na shughuli ya kukata na kuunganisha madirisha kwenye banda la VETA, Sabasaba.

RAFAEL Mwambalaswa, ni Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam(UDSM) anayefundisha saikolojia.

Mwambalaswa ana ulemavu wa kutokuona, ambaye amelazimika kufanya utafiti kwa kufanya kazi za mikono za ufundi wa kutengeneza madirisha kupitia Chuo cha  Mafunzo ya Ufundi Stadi(VETA) cha Dar es Salaam..

Anasema lengo la kufanya utafiti katika eneo hilo ni kutaka kubaini kama endapo upo uwezekano wa mtu mwenye ulemavu wa kutokuona au yeyote mwenye mahitaji maalum kupata ujuzi hususani wa ufundi wa kutumia mikono ambao unaweza kumwezesha kujiajiri au kuajiriwa halafu akapata kipato cha kiendesha maisha yake.

Mwambalaswa alizungumza hayo na Nipashe katika banda la Veta kwenye maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Dar es Salaam(DITF), yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba, Temeke.

"Kwa hiyo mpaka sasa nimejifunza kwa miezi mitatu na ninatakiwa nijifunze kwa miezi sita, lakini tayari nimebaini kwamba inawezekana kwa mtu mwenye ulemavu wa macho au ulemavu mwingine wowote kufanya shughuli hizi za ufundi,"anasema Mwambalaswa.

"Kwa kipindi ambacho nimefika Veta tayari ninaweza kufanya shughuli zangu za ufundi vizuri na ninatengeneza madirisha bila utegemezi wa mtu yeyote licha ya kwamba sioni. Kwa hiyo niliona  niwatie moyo watu wenye uelemavu kama wangu kwamba inawesekana kufanya shugjuli yoyote ukiamua, watafute mafunzo wapate ujuzi ili wafanye shughuli za kujiingizia kipato."